Friday, May 30, 2014

KAPOMBE ASAINI MITATU AZAM

Posted By: Unknown - 6:00 AM

Share

& Comment

Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
HATIMAYE klabu ya Azam FC imefanikiwa kumsajili, beki anayeweza kucheza nafasi za kiungo pia, Shomary Salum Kapombe baada ya jana kumsainisha Mkataba wa miaka mitatu. 

Katibu wa Azam FC, Nassor Idrissa Mohammed ‘Father’ ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, wamefuata taratibu zote kabla ya kumsainisha mchezaji huyo, na kufanikiwa kumalizana na klabu yake, AS Cannes ya Ufaransa.

“Kama inavyofahamika, mchezaji huyu alihamishwa kutoka Simba SC kwenda AS Cannes mwaka jana, kwa hivyo nasi tumemsajili kutoka timu hiyo, lakini asilimia fulani ya fedha, ambazo tutawalipa Simba SC,”amesema Nassor.
Maisha mapya; Shomary Kapombe kulia sasa ni mchezaji wa Azam FC 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema; “Hatuna tatizo na Kapombe, awaambie Azam FC walete asilimia 40 yetu katika fedha walizotoa kumnunua huko Cannes, na sisi tutanunua wachezaji wengine wazuri tu hata wawili kwa hiyo fedha,”.

Tayari Kapombe alikuwa amekwishajiunga na Azam FC tangu Machi mwaka huu baada ya kugoma kurejea Ufaransa tangu Novemba mwaka jana aliporejea kuichezea timu ya taifa, Taifa Stars mchezo wa kirafiki dhidi ya Zimbabwe.  

Kapombe aliyezaliwa Januari 28, mwaka 1992 aliibukia katika timu ya vijana ya Polisi Morogoro kabla ya kusajiliwa na Simba mwaka 2011, ambako alicheza hadi Agosti mwaka jana alipojiunga na Cannes.

Simba SC ilimtoa mchezaji huyo bure AS Cannes kwa makubaliano akiuzwa klabu nyingine, itapata mgawo mzuri.

Hata hivyo, baada ya kugoma kuendelea kuchezea klabu hiyo ya Daraja la Nne, Simba SC ilitakiwa kulipa Euro 33, 000 ambazo sawa na Sh. Milioni 66 ili kurejeshewa mchezaji wake huyo.

Kapombe anakuwa mchezaji wa tano kusajiliwa na mabingwa hao wapya wa Ligi Kuu, baada ya beki Abdallah Kheri kutoka Zimamoto ya Zanzibar kiungo Frank Domayo na washambuliaji Mrundi Didier Kavumbangu kutoka Yanga na Ismaila Diarra kutoka Mali. 


CHANZO: BIN ZUBEIRY

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.