TIMU za Azam FC na JKT Ruvu za chini ya miaka 20, zinatarajiwa kutoa ushindani katika michuano ya Kombe la Fasdo inayoanza kutimua vumbi leo Jumatatu kwenye Uwanja wa Bandari, uliopo Temeke jijini Dar es Salaam.
Michuano hiyo imeandaliwa na Faru Arts and Sports Organisation (Fasdo) kwa kushirikiana na Chama cha Soka Temeke(TEFA). Timu 16 kutoka mikoa mbalimbali nchini zitakazochuana.
Mkurugenzi wa Fasdo, Tedvan Chande, alizitaja baadhi ya timu zitakazoshiriki kuwa ni Azam FC, Ruvu JKT, Twalipo, Kiombo, Kitunda, Dar Youth na Kijichi.
“Wachezaji 25 watatafutiwa timu kama utekelezaji wa kauli mbiu ya michuano hiyo ili waweze kufaidika na vipaji vyao, tunachoomba ni wachezaji wenyewe kujitambua kuwa soka ni kazi na ajira yao,” alisema.
Alisema zawadi kwa timu itakayokuwa bingwa ni Sh2 milioni, huku washindi wa pili wakipata Sh1 milioni na wa tatu watapewa 500,000. Kutakuwa pia na zawadi kwa Mfungaji Bora.
0 Maoni:
Post a Comment