
KOCHA Mkuu wa Azam FC, Joseph Omog amesema kikosi chake kimeimarika kwa kiasi kikubwa na ndio maana kimepata ushindi dhidi ya El Merreikh ya Sudan wa mabao 2-0 juzi katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Katika mchezo huo wa raundi ya awali, Azam FC walicheza mchezo mzuri na kwa kujiamini kiasi cha kuwabana wapinzani wao kwa kupata ushindi huo kwa mabao ya washambuliaji Didier Kavumbagu na John Bocco.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Omog alisema kikosi chake kilicheza vizuri na kwa kujituma ndio maana walifanikiwa kuwabana wapinzani wao kwa kupata ushindi huo mkubwa.
“El Merreikh ni timu nzuri, ndio maana tulifanya maandalizi makubwa kuhakikisha tunautumia uwanja wetu wa nyumbani vizuri kwa ajili ya kushinda,” alisema kocha huyo raia wa Cameroon.
Alisema kikubwa kilichosababisha kushindwa kufanya vizuri katika baadhi ya mechi zilizopita zikiwemo za Ligi Kuu, ilikuwa ni kushindwa kufunga, lakini sasa wamepata dawa ya tatizo hilo huku akiahidi kuendelea kulitatua limalizike.
Alisema tatizo la ufungaji wataendelea kulifanyia kazi kila siku ili kuhakikisha wanaendelea kufanya vizuri katika michezo mbalimbali ijayo.
Alisema katika kuhakikisha wanaitoa El Merreikh katika mchezo wa marudiano siku chache zijazo, wataendelea na mazoezi ya nguvu na taratibu kiwango chao kitaonekana.
Kwa upande wa Kocha wa El Merreikh, Diego Garzitto alikilaumu kikosi chake kwa kushindwa kutumia nafasi walizokuwa wakizipata katika kufunga licha ya kuwa na uzoefu katika michuano hiyo kwa muda mrefu.
Alisema wana kazi kubwa ya kuhakikisha mchezo wa marudiano utakaopigwa kwao, wanashinda ili kusonga mbele.
“Tunahitaji kubadilika katika mchezo wa marudiano, mchezo wa kasi utatusaidia kupata matokeo mazuri, tumepoteza ugenini tunaangalia mbele ni kwa vipi tujipange,” alisema.
Chanzo: habari leo
0 Maoni:
Post a Comment