Saturday, December 12, 2015

AZAM NA SIMBA HAKUNA MBABE

Posted By: kj - 10:30 PM

Share

& Comment


MABINGWA wa Kombe la Kagame, timu ya Azam FC leo imeenda sare ya mabao 2-2 na Simba katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jioni hii.

Licha ya sare hiyo, Azam FC imeendelea kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi ikijiongezea pointi moja na kufikisha 26 huku Yanga inayoafutia iliyotoa suluhu dhidi ya Mgambo JKT leo ikifikisha alama 24.

Shukrani za pekee ziende kwa nahodha wa Azam FC, John Bocco ‘Adebayor’, aliyefunga mabao yote, huku Ibrahim Ajibu naye akifanya hivyo kwa upande wa Simba.

Azam FC iliuanza vema mchezo huo kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la kwanza katika sekunde ya 50, lililofungwa na Bocco, aliyemzidi maarifa kipa wa Simba, Vincent Angban, kufuatia pasi ya winga Farid Maliki.

Maliki alifanya kazi ya ziada kabla ya bao hilo baada ya kumpora mpira beki wa kulia wa Simba, Emery Nimubona.

Vinara hao wa ligi waliendelea kulisakama lango la Simba kwa takribani dakika saba za mwanzo, kabla ya wekundu hao kuamka na kufanikia kupata bao la kusawazisha dakika ya 25 kupitia kwa mshambuliaji Ibrahim Ajibu.

Hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zimalizika timu hizo zilikwenda vyumbani zikiwa nguvu sawa kwa mabao hayo huku kipa wa Azam FC, Aishi Manula, akionekana kufanya kazi kubwa ya kuokoa michomo hatari ya Simba.

Kipindi cha pili kilianza kwa Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, kufanya mabadiliko kwa kumtoa kiungo Himid Mao ‘Ninja’ na nafasi yake kuchukuliwa na Muivory Coast, Michael Bolou.

Mabadiliko hayo yaliisaidia Azam FC kwani ilirejea mchezoni, ambapo Bolou alionekana kushirikiana vema na mwenzake Jean Baptiste Mugiraneza ‘Migi’, kwenye eneo la ukabaji.  

Ajibu alifanikiwa kuipatia Simba bao la pili dakika ya 68 baada ya kutokea uzembe kwenye eneo la ulinzi, lakini Azam FC ilirejea kwa kasi kubwa na kusawazisha bao hilo kupitia kwa Bocco dakika ya 73.

Bocco alifunga bao hilo kwa ustadi mkubwa baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Kipre Tchetche, aliyepokea pasi safi ya kifua kutoka kwa Didier Kavumbagu, aliyeingia dakika ya 71 kuchukua nafasi ya kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’.

Tchetche alikaribia kuiandikia Azam FC bao la tatu dakika ya 76 baada ya kuwahadaa mabeki wa Simba na kupiga shuti kali lililogonga mwamba wa chini na mpira kumrudia kipa Angban, aliyeudaka.

Hadi dakika 90 za mwamuzi Erick Onoka kutoka Arusha zinamalizika matokeo yalibakia kwa sare hiyo.

Mara baada ya mchezo huo kumalizika, Kocha wa Azam FC, Stewart Hall, aliuambia mtandao wa azamfc.co.tz, kuwa mechi wa kwanza kwa timu baada ya mapumziko ya mechi za timu ya Taifa huwa ni ngumu kwa makocha.

“Azam tulikuwa na timu nne tofauti zilizokuwa na wachezaji wetu kwenye michuano ya CECAFA (Kombe la Chalenji), idadi kubwa kuliko timu nyingine yoyote, wiki hii tulifanya mazoezi kama wageni, wachezaji wangu wengi walikuwa nje ya timu kwa muda wa mwezi mzima.

“Kila kitu kilishindwa kwenda vizuri, kila mmoja alijiona mgeni, yote haya yamechangia kuathiri kiwango chetu leo, nilihitaji mchezo mwepesi kidogo kwa wachezaji wangu ili kuwarudisha kwenye hali ya kuzoeana,” alisema.

“Simba ilicheza vizuri dakika 25 za mwisho za kipindi cha kwanza, walicheza kwa haraka pasi moja, mbili, nadhani tulikuwa na matatizo kwenye ulinzi, lakini tulicheza vema sana kipindi cha pili,” alisema Hall.

Naye Bocco alisema kuwa mchezo huo ulikuwa mgumu sana, lakini waliweza kupambana huku akimshukuru Mungu kwa kufunga mabao mawili yaliyoiwezesha Azam FC kupata pointi moja.

“Tunamshukuru Mungu kwa kupata pointi moja na mimi kufunga mabao yaliyoiwezesha timu yangu kuzoa pointi hiyo, mchezo ulikuwa mgumu, lakini kuelekea mchezo ujao (Majimaji) tutachukua pointi tatu kwani kila mchezo ni muhimu kwetu,” alisema.

Azam FC inatarajia kushuka tena dimbani Desemba 20 mwaka huu kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea kuvaana na timu ya Majimaji ya huko, ambayo leo imepigwa mabao 5-1 na Toto Africans.

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.