Monday, November 4, 2013

KUELEKEA NOV 7: HALL MBEYA CITY WALO VIZURI

Posted By: azam fans - 10:56 PM

Share

& Comment

WAKATI mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom ukitarajiwa kufikia tamati Novemba 7, kocha wa wana lambalamba Azam FC, Stewart Hall, amekiri mechi yao ya kukamilisha ngwe hiyo dhidi ya Mbeya City inampa mawazo.

Hall raia wa Uingereza, alisema jijini Dar es Salaam jana kwamba, hakuna timu anayoihofia katika Ligi Kuu kama Mbeya City inayonolewa na kocha mzawa, Juma Mwambusi, kutokana na uwezo wa mchezaji mmoja mmoja na kitimu pia.

Alisema ana imani mechi dhidi yao itakuwa ngumu, hivyo anajipanga kuhakikisha ubora wa kikosi chake unaipa timu ushindi katika mchezo huo utakaopigwa Azam Complex, Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam na kuendelea kushika usukani wa ligi hiyo.

“Mimi naamini kila timu ambayo inacheza Ligi Kuu ni nzuri na ina uwezo hadi kufikia hatua hii, ila hakuna timu ambayo naiogopa, isipokuwa Mbeya City ni wazuri na ndiyo maana nasema itakuwa mechi ngumu kwangu, lakini nimejipanga na naendelea kujipanga ili kushinda mchezo huo,” alisema Hall.

Aidha, aliwapongeza vijana wake kwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Ruvu Shooting juzi na kuwataka wasibweteke, kwa kuwa safari ndiyo kwanza imeanza na lengo lake ni kutwaa ubingwa msimu huu unaoshikiliwa na Yanga.

Azam FC iko kileleni mwa ligi hiyo wakiwa na pointi 26 sawa na Mbeya City, lakini wakizidiana wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa, huku Yanga ikifuatia kwa pointi 25 na Simba 21.

Mechi za kukamilisha mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo zitachezwa Novemba 6 na 7.

Novemba 6 JKT Ruvu watamenyana na Coastal Union Azam Complex, Ashanti United na Simba Uwanja wa Taifa, Kagera Sugar dhidi ya Mgambo Shooting Kaitaba huku Ruvu Shooting na Mtibwa Sugar watapepetana Uwanja wa Mlandizi Mabatini.

Novemba 7, Azam watawakaribisha Mbeya City Chamazi, Yanga na Oljoro JKT Uwanja wa Taifa Dar es Salaam wakati Rhino itakuwa mwenyeji wa Tanzania Prisons Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi, Tabora.


CHANZO: TANZANIA DAIMA

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.