Fuatilia ripoti kamili ya mchezo kwa hisani ya gazeti la Mwananchi na picha kwa hisani ya blogu ya Bin Zubeiry hapa chini
PASI fupifupi, mashambulizi ya kushitukiza, kasi na uzoefu wa michuano ya Kombe la Kagame, umeiwezesha Yanga kutwaa ubingwa huo kwa mara ya tano ikiwa ni mwaka mmoja pungufu ya Simba inayoshikilia rekodi ya kutwaa mara sita.
Yanga iliyoingia kwenye michuano ya mwaka huu kama mabingwa watetezi, walianza kutwaa ubingwa 1975 kwa kuifunga Simba 2-0 katika fainali mjini Zanzibar.
Ilitwaa tena ubingwa 1993 kwa kuilaza 2-1 SC Villa ya Uganda michuano ilifanyika Uganda sawa na 1999, kwa mara ya pili, ilirudi na kombe kutoka Uganda.
Baada ya sare ya 1-1 dakika 120, Yanga iliifunga SC Villa mikwaju ya penalti 4-1. Mwaka 2011 Yanga ilinyakua ubingwa kwa kuilaza Simba bao 1-0 katika mechi ya fainali, michuano iliyofanyika Tanzania.
Yanga iliyokuwa Kundi C na Atletico Olympio (Burundi), APR (Rwanda) na Wau Salaam ya Sudan iliilaza Azam FC, wageni wa michuano hiyo kwa mabao mabao 2-0, shukrani kwa mabao ya kila kipindi kutoka kwa Hamis Kiiza na Said Bahanuzi.
Mechi hiyo ya fainali ilikuwa na maana nyingi, kwanza Yanga imelipa kisasi cha kufungwa mabao 3-1 katika mechi ya Ligi Kuu Bara ambayo Wanajangwani hao waliishia kumpiga mwamuzi, Israel Nkongo.
Azam walitawala mchezo dakika 20 za kwanza, kabla ya kibao kugeuka na kuipa Yanga fursa ya kutawala mchezo kwa mashambulizi ya kushtukiza na mashuti ya mwendo mrefu.
John Bocco aliyefunga mabao yote matatu katika ushindi wa 3-1 dhidi ya Simba hatua ya robo fainali, jana alishikwa vilivyo na ngome ya Yanga chini ya Nadir Haroub na Kelvin Yondan.
Alifanya majaribio makubwa mawili langoni mwa Yanga katika nusu ya kwanza, dakika ya pili baada ya shuti lake kushindwa kulenga lango kufuatia krosi ya Erasto Nyoni.
Angeweza kufanya matokeo kuwa 1-0 dakika 12 baadaye kama siyo mpira wake wa kichwa uliotokana na kona ya Salum Aboubakari usingemgonga miguu ya kipa Ali Mustapha wa Yanga.
Kipa wa Azam, Deogratius Munishi alifanya kazi ya zaida kupangua shuti la Haruna Niyonzima, huku Rashid Gumbo naye akishindwa kuzitungua nyavu za Azam dakika ya 25.
Erasto Nyoni alimjaribu Mustapha kwa shuti kali ya kushitukiza nje ya eneo la hatari, lakini hata hivyo halikuweza kulenga lango.
Mshabiki wa Yanga walinyanyuka kwenye viti vyao kushangilia bao la utangulizi likifungwa na Hamis Kiiza dakika ya 44.
Kiiza alifunga bao hilo kwa shuti lililopenya katikati ya miguu ya kipa Munishi, akitumia makosa ya beki Aggrey Morris alirusha pasi fupi iliyonaswa na Kiiza.
Shujaa aliyehakikisha ubingwa unabaki Jangwani, alikuwa mshambuliaji mpya Bahanuzi, aliyefunga bao la pili kwa shuti kali sekunde chache kabla ya kumalizika mpira.
Bahauzi alifunga bao hilo zuri, akipokea pasi ndefu ya Yondani na kumpiga chenga Said Morad kabla ya kuzitingisha nyavu za Azam, huku Munisi akiruka kuzuia mpira bila mafanikio.
Katika mchezo huo, mwamuzi Thiery Nkurunziza wa Burundi aliyelimudu pambano hilo, aliwaonyesha kadi za njano, Bahanuzi na Mustapha kwa upande wa Yanga na Jabir wa Azam.
Kipindi cha pili kilitawaliwa na Yanga iliyokuwa ikitumia mfumo wa 5-3-2, na wapinzani wao wakicheza wakitumia 5-3-2.
Beki Mwasika wa Yanga aliinyima Azam bao baada ya kuucheza mpira uliokuwa tayari umeshampita kipa wake katika dakika ya 57.
Yanga ingeweza kuondoka na ushindi mkubwa kama washambuliaji wake wangetumia vizuri nafasi walizopata, ikiwamo ya Niyonzima kuingia ndani ya 18 na kufumua shuti lililopaa juu kidogo ya lango katika dakika ya 82.
Katika mchezo huo, Azam walifanya mabadiliko kwa kumtoa Kipre na nafasi yake kuchukuliwa na Mrisho Ngasa dakika ya 67, na kisha kuingia Samir Nuhu kuchukua nafasi ya Shikanda, huku Yanga akitoka Rashid Gumbo na kuingia Juma Seif katika dakika ya 75.
Mabadiliko hayo yalikuwa nafuu zaidi kwa Yanga iliyocheza kwa kuelewana na kutawala sehemu kubwa ya kipindi cha pili ambacho wachezaji wa Azam walionekana kuchoka.
Kocha wa Azam, Hall Stawart alikubali kipigo hicho alichosema kimetokana na makosa yaliyofanya na mabeki wake.
"Katika soka mambo haya yanatokea, ukifanya kosa mwenzako analitumia vizuri kufunga, ndivyo walivyofanya Yanga. Mchezo ulikuwa mgumu, lakini nimeridhika na matokeo," alisema.
Naye kocha wa Yanga, Tom Saintifiet alisema: "Sina la kusema zaidi ya kupongeza vijana wangu, wamefanya kazi nzuri na kutwaa ubingwa...mechi ilikuwa ngumu," alisema.
Awali kabla ya mchezo huo, AS Vita ya DR Congo iliilaza APR ya Rwanda mabao 2-1 mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu na nne.
AS Vital walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa Magola Mapanda kwa shuti kali lililomshinda kipa wa APR, Ndayishimiye Jean Luc katika dakika ya 18.
Bao la pili lilifungwa dakika ya 67 kupitia kwa Mutombo Kazadi. Bao la kufutia machozi la APR lilifungwa na Mugiraneza Jean .
Source; http://www.mwananchi.co.tz/michezo/-/25126-ni-yanga-tena-kagame
http://bongostaz.blogspot.com/
0 Maoni:
Post a Comment