Thursday, December 15, 2016

WATATU WAZMWAGA WINO AZAM FC

Posted By: kj - 11:58 AM

Share

& Comment


UONGOZI wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, unayofuraha kuutarifu umma kuwa leo mchana imefanikiwa kuingia mkataba na wachezaji watatu, beki wa kati Yakubu Mohammed, kiungo mkabaji Stephan Kingue Mpondo na winga Joseph Mahundi.

Zoezi hilo la kuingiana mikataba limehudhuriwa na baadhi ya viongozi wakuu wa timu wakiwemo Ofisa Mtendaji Mkuu, Saad Kawemba, Meneja Mkuu, Abdul Mohamed, Kocha Mkuu Zeben Hernandez, Meneja wa timu, Phillip Alando.

Wakati Mohammed, 20, amesaini mkataba wa miaka mitatu akitokea Aduana Stars ya Ghana, utakaomuweka kwenye viunga vya Azam Complex hadi Desemba 14, 2019 akiziba nafasi ya Pascal Wawa, huku Mpondo anayetokea Coton Sports ya Cameroon, kwa upande wake akisaini mwaka mmoja.

Nyota hao wawili wamepewa rasmi mikataba baada ya kulivutia benchi la ufundi la Azam FC kwenye majaribio waliyokuwa wakifanya ndani ya kikosi hicho.

Katika kuongeza makali kwenye eneo la ushambuliaji, Azam FC imemrejesha winga wake wa zamani aliyekulia Azam Academy, Mahundi, ambaye amesaini miaka miwili akitokea Mbeya City, alipomaliza mkataba baada ya kumalizika kwa raundi ya kwanza ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Azam FC tunaamini ya kuwa ujio wa nyota hao, utazidi kuipa nguvu timu yetu kuelekea mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) unaotarajia kuanza wikiendi hii, Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) na Kombe la Shirikisho Afrika (CC) mwakani.

Hivyo mashabiki wa Azam FC wasiwe na wasiwasi waendelee kuisapoti timu, kwani bado uongozi wa timu kwa kushirikiana na benchi la ufundi, una nia ya dhati ya kuipeleka mbele timu kufikia kwenye mafanikio yanayokusudiwa kwa kukiboresha kikosi kadiri inavyowezekana.

Wakati huo huo, Azam FC inapenda kuweka wazi taarifa ya kufikia makubaliano ya kuachana na kiungo mkabaji raia wa Rwanda, Jean Baptiste Mugiraneza ‘Migi’, ambaye amepata timu nchini Vietnam na muda wowote kuanzia sasa atakwenda huko.

Azam FC inamtakia mafanikio mema Migi huko aendako na inapenda kumkaribisha muda wowote atakapojisikia kurejea tena hapa na katika kuziba nafasi yake tumeamua kumsajili Mpondo, ambaye alikuwa nahodha wa timu ya Taifa ya Cameroon kwenye kikosi kilichoshiriki Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) zilizofanyika nchini Rwanda mwanzoni mwa mwaka huu.   

Imetolewa na Uongozi wa Azam FC
Desemba 14, 2016.

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.