Saturday, October 7, 2017

AZAM FC WAICHAPA MOJA NGORONGORO

Posted By: kj - 5:20 PM

Share

& Comment

KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imeichapa timu ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ‘Ngorongoro Heroes’ bao 1-0 katika mchezo wa kirafiki wa mazoezi uliofanyika Uwanja wa JMK Park leo asubuhi.

Mchezo ulikuwa ni maalum kwa ajili ya vikosi vyote viwili kujipima, Azam FC ikijiwinda na mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Mwadui utakaofanyika Uwanja wa Mwadui Complex Oktoba 14 mwaka huu.

Ngorongoro inaendelea na kambi ya wiki kadhaa kujitayarisha na mechi za kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana zitakazofanyika nchini Niger mwaka 2019, ambapo benchi la ufundi la timu hiyo chini ya Mdenmark, Kim Poulsen, lipo kwenye mchujo wa kutafuta kikosi kamili.

Mtanange huo ulikuwa ni kukata na shoka, timu zote zikifanikiwa kuonyeshana ushindani wa kweli jambo ambalo linaleta mwanga mzuri kwa hapo baadaye kwa kikosi hicho cha vijana.

Bao pekee la Azam FC kwenye mchezo huo limefungwa na Nahodha Msaidizi, Agrey Moris, kwa njia ya mkwaju wa penalti dakika ya 63 baada ya winga Enock Atta kuangushwa ndani ya eneo la hatari

Kocha Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba, aliweza kupanga vikosi viwili katika mchezo huo, cha kwanza kilichosheheni wachezaji ambao hawajacheza mechi nyingi kilianza kipindi cha kwanza huku kile cha kila siku kikiingia kipindi cha pili.

Jumla ya wachezaji wanne wa Azam U-20 katia ya sita walioitwa kwenye kikosi cha Ngorongoro, waliweza kucheza katika mchezo huo, wawili wakianza ambao ni beki wa kati Oscar Masai, beki wa kushoto Said Issa ‘Shilla’ wengine wakiingia kipindi cha pili kiungo Rajab Odasi na mshambuliaji Paul Peter.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kitaendelea tena na mazoezi kesho Jumapili jioni tayari kabisa kufanya mazoezi ya mwisho mwisho kabla ya kuelekea mkoani Shinyanga kukipiga na Mwadui na baadaye mkoani Mwanza kumenyana na Mbao Oktoba 21, mwaka huu.

Kikosi cha Azam FC leo:

Mwadini Ally/Benedict Haule dk 46, Abdul Omary/Swaleh Abdallah dk 46, Hamimu Karim/Bruce Kangwa dk 46, David Mwantika/Yakubu Mohammed dk 46, Abdallah Kheri/Agrey Moris dk 46, Salmin Hoza/Daniel Hoza dk 46, Ramadhan Singano/Idd Kipagwile dk 46, Masoud Abdallah/Salum Abubakar dk 46, Wazir Junior/Yahya Zayd dk 46, Joseph Mahundi/Enock Atta dk 46

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.