NAHODHA wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, John Bocco ‘Adebayor’, juzi jioni alizidi kuingia kwenye vitabu vya rekodi vya timu hiyo baada ya kufunga bao la kusawazisha dakika za mwisho, lililowafanya kuingia hatua ya matuta na kutwaa taji la kwanza la Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga.
Bocco alifunga bao hilo dakika ya 90 kwa njia ya mkwaju wa penalti baada ya beki wa Yanga, Vicent Bossou, kuunawa mpira akiwa nani ya eneo hatari na kufanya muda wa kawaida kuisha kwa sare ya mabao 2-2.
Kama hiyo haitoshi Bocco ambaye ni takribani mwaka wa nane hivi sasa anaichezea Azam FC, ndiye aliyefunga penalti ya ufunguzi ya timu hiyo kwenye hatua ya matuta, ambayo iliweza kuwafungulia njia wachezaji wenzake na kushinda kwa mikwaju ya penalti 4-1.
Rekodi zake nyingine
Wakati akiwa mfungaji bora wa Azam FC wa muda wote, Bocco pia ameweka rekodi nyingine tatu zilizoweza kuipa mafanikio Azam FC hadi inafika hatua hii.
Julai 27, 2008, Bocco aliianzisha vema safari ya mafanikio ya Azam FC wakati huo ikinolewa na Mohamed Seif ‘King’, baada ya kufunga mabao mawili yaliyoipandisha daraja hadi Ligi Kuu, ilipocheza Majimaji ya Songea kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma.
Azam FC ilipanda daraja baada ya kufikisha jumla ya pointi saba kuongoza kituo cha mkoa wa Dodoma na kuzizidi kete Majimaji, Kijiweni FC ya Mbeya na Mbagala Market ya Dar es Salaam (hivi sasa African Lyon).
Nahodha huyo alirejea tena msimu wa 2011/2012 na kuandika rekodi ya kuwa mfungaji bora wa pili wa ligi aliyetokea Azam FC baada ya kufunga mabao 19, akimfuatia Mrisho Ngassa aliyetupia 16 2010/11.
Nyota huyo wa zamani wa timu ya Cosmopolitan, alifanikiwa kufunga bao la ushindi lililoipa Azam FC ubingwa wa Ligi Kuu msimu 2013/14, ikiichapa Mbeya City mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya bao jingine likifungwa na Gaudence Mwaikimba. ikitwaa kwa rekodi ya aina yake ya bila kufungwa mchezo wowote.
Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB na kinywaji safi cha Azam Cola, ilitwaa ubingwa huo Aprili 13, 2014 kwa rekodi ya aina yake ya bila kufungwa mchezo wowote ndani ya mechi zote 26 za ligi.
Agosti 2, mwaka jana, wakati Azam FC ikitwaa ubingwa wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Kagame Cup), Bocco ndiye aliyefungua ukurasa wa timu hiyo katika mechi ya fainali dhidi ya mabingwa wa Kenya Gor Mahia, akifunga bao la kwanza kwenye ushindi wa 2-0, jingine likifungwa na Kipre Tchetche, kwa mpira wa moja kwa moja wa adhabu ndogo.
Bocco anena
Akianza kuzungumzia ubingwa wa Ngao ya Jamii, Bocco aliwapongeza wachezaji wenzake kwa kupambana kwenye mchezo hadi kuibuka mabingwa, huku akisema hiyo ni ishara nzuri kwao ya kufanya vema msimu ujao.
“Ni kweli kipindi cha kwanza hatukuanza vizuri sana, lakini mpira ni mchezo wa makosa, jinsi mnavyofanya makosa wenzezu ndio wanapoyatumia, kipindi cha pili tulirudi baada ya kocha kutupa maelekezo na hatimaye tukarekebisha makosa na kushinda mchezo huo,” alisema.
Bocco alisema hiyo ni zawadi nyingine kwa klabu yake, na kueleza kuwa atazidi kujituma kila siku ili kuipa mafanikio zaidi huku akimshukuru Mwenyezi Mungu kwa mambo mazuri anayoendelea kuyafanya.
0 Maoni:
Post a Comment