Sunday, October 16, 2016

AZAM WATOKA SARE NA YANGA

Posted By: dada - 9:32 PM

Share

& Comment

IKICHEZA soka zuri la kuvutia na kuwatawala sehemu kubwa ya mchezo, Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imetoka sare ya bila kufungana na Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliofanyika jioni ndani ya Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Mbali na kutawala mchezo, Azam FC ilifanikiwa pia kutengeneza nafasi nyingi za kufunga mabao, lakini tatizo kubwa liliendelea kuwa ni umaliziaji baada ya nafasi zaidi ya tatu kupotezwa.

Matokeo hayo yanaifanya Azam FC kufikisha jumla ya pointi 12 kwenye msimamo wa ligi baada ya kucheza mechi tisa, ikishinda tatu na sare tatu.

Alikuwa ni Gonazo Ya Thomas, aliyepata nafasi ya kwanza akiwa ndani ya eneo la 18 kufuati kupewa pasi safi na Mudathir Yahya lakini shuti alilopiga lililotoka sentimita chache ya lango la Yanga.

Azam FC iliendelea kuliandama lango la Yanga ambapo madhambi aliyofanyiwa winga Bruce Kangwa na beki Kelvin Yondani pembeni kidogo ya lango la Yanga, almanusura yazae bao dakika ya 23 baada ya Mudathir kupiga faulo nzuri iliyopanguliwa na kipa wa Yanga, Deogratius Munishi ‘Dida’ na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Bocco alifanya jitihada binafsi dakika ya 41 baada ya kumuhadaa Haji Mwinyi na kupiga shuti kali lililopanguliwa na kipa wa Yanga na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika timu zote ziliweza kwenda nguvu sawa bila kufungana. Azam FC ilianza kwa kasi kubwa kipindi cha pili ikipiga presha kubwa langoni mwa Yanga.

Azam FC ilifanya shambulizi kali langoni mwa Yanga dakika ya 48 baada ya Thomas kumzidi maarifa Mbuyu Twite wa Yanga na kupiga pasi nzuri ndani ya eneo la 18, lakini Mudathir alishindwa kuuwahi mpira na kudakwa na kipa wa Yanga.

Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii, walizidi kuuutawala mchezo huo kwa kipindi cha pili na kupeleka kasi ya mashambulizi langoni mwa Yanga, hasa kasi ikaongeza zaidi baada ya kuingia kiungo Frank Domayo na mshambuliaji Fransisco Zekumbawira na kutoka Mudathir na Bocco.

Domayo alikaribia kuiandikia bao la uongozi Azam FC dakika ya 83 baada ya kupiga kichwa kizuri kilichogongwa mwamba na kurudi uwanjani kufuatia kona iliyochongwa na Erasto Nyoni.

Matokeo ya mchezo huo yanafanya rekodi ya timu hizo mbili kuendelea kuwa nguvu sawa baada ya kulingana kila kitu kwenye mechi zote 17 walizocheza kwenye ligi.

Ndani ya mechi hizo, Azam FC imeshinda mechi tano sawa na Yanga huku zikienda sare mara saba na kila upande ukiwa umemfunga mwenzake mabao 25.

Mara baada ya mchezo huo kikosi cha Azam FC kitaendelea tena na mazoezi kesho jioni kujiandaa na mchezo ujao wa ligi dhidi ya Mtibwa Sugar utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Jumatano ijayo.

Kikosi cha kilichocheza:

Aishi Manula, Himid Mao, Erasto Nyoni, Daniel Amoah, Aggrey Morris, Jean Mugiraneza, Bruce Kangwa/Khamis Mcha dk 87, Salum Abubakar, John Bocco (C)/Francisco Zekumbawira dk 77, Mudathir Yahya/Frank Domayo dk 69, Gonazo Ya Thomas

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.