Thursday, August 23, 2012

AZAM KUJIPIMA KWA PRISONS

Posted By: azam fans - 3:33 PM

Share

& Comment



Azam FC

Na Mahmoud Zubeiry
KATIKA kujiandaa na mechi ya Ngao ya Jamii, washindi wa pili wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Azam FC Jumamosi watamenyana na Transit Camp kwenye Uwanja wa Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Habari kutoka Azam, zimesema kwamba kabla ya mchezo huo, kesho Azam katika kuwakomaza wachezaji wake wa timu ya vijana, Azam Academy watacheza mechi ya kujipima nguvu na Prisons ya Mbeya, iliyorejea Ligi Kuu msimu huu.

Azam ambayo ipo chini ya kocha mpya, Mserbia Boris Bunjak, inatarajiwa kuivaa Simba katika mechi ya Ngao ya Jamii ya kuashiria kufunguliwa kwa pazia la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Septemba 8, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam..

Habari za ndani kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), zimesema kwamba, kuchelewa kwa mechi hiyo ambako kumeenda sambamba na kuchelewa kuanza kwa ligi hiyo, kumetokana na kuchelewa kufikiwa mwafaka mapema wa mkataba mpya wa udhamini wa Ligi Kuu.

Mkataba wa awali wa Vodacom na TFF unafikia tamati mwishoni mwa mwezi huu na kusainiwa mkataba mwingine, baada ya majadiliano yanayoendelea.

Lakini kwa kuwa Mkutano Mkuu wa TFF uliopita uliridhia kuanzia msimu ujao Ligi Kuu iendeshwe na kampuni itakayoundwa na klabu za Ligi Kuu mjadala kuhusu udhamini mpya wa ligi umekuwa mrefu kutokana na kuhusisha pande tatu, klabu, wadhamini na shirikisho.

Lakini sasa, kwa vyovyote, hata maridhiano ya mkataba mpya wa udhamini na Vodacom yachelewe tena, mechi hiyo itachezwa Septemba 8, ikiwa ni wiki moja kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu.

Kihistoria hiyo itakuwa mechi ya tano ya Ngao ya Jamii kuchezwa nchini na ya pili kuishirikisha timu nje ya wapinzani wa jadi wa soka ya Tanzania, Simba na Yanga.

Mtibwa ilicheza na Yanga mwaka 2009, baada ya Simba kugoma na ikashinda mabao 2-1 na kutwaa Ngao, wakati kabla ya hapo, mwaka 2001, Ligi Kuu ya Tanzania ikiwa bado inadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Safari Lager, ilichezwa mechi ya kwanza ya Ngao kihistoria.

Katika mechi hiyo, Yanga ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Simba na mwaka juzi Yanga iliifunga tena Simba kwa penali 3-1 kufuatia sare ya 0-0 na mwaka jana, Simba ilitwaa Ngao ya kwanza katika historia yake, kwa kuifunga Yanga mabao 2-0.


Source: BIN ZUBEIRY

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.