Klabu ya Azam FC inapenda kutoa taarifa ya ufafanuzi juu ya sakata la mchezaji Mrisho Ngasa ambalo linaonekana kupotoshwa
1. Azam FC ilitangaza kuwa biashara ya mchezaji Mrisho Ngasa ingefungwa siku ya Jumatano 1/08/2012 saa saba mchana na ilivitaka vilabu vyenye interest na mchezaji huyo kufika makao makuu ya Azam FC ofisi ndogo zilizopo kwenye kiwanda cha unga cha Azam-Mzizima zikiwa na pesa taslimu. Bei ya mauzo iliyopangwa ilikuwa ni Dola 50,000. Lakini katika mawasiliano ya email kwa makatibu wakuu wa Simba na Yanga, Azam FC iliweka bayana kuwa ilikuwa tayari kushusha bei ya mauzo na ingemuuza Ngasa kwa timu ambayo dau lake lingekuwa kubwa zaidi ya mwenzake.
Kwa maana hiyo biashara ya mchezaji mrisho ngasa ilifanyika kwa uwazi. Lengo la Azam FC lilikuwa ni kutoa haki kwa kila klabu yenye uwezo wa kifedha kuweza kupata huduma ya Ngasa.
Pia tunaomba ifahamike bayana kuwa mchezaji Mrisho Ngasa alipewa taarifa kuwa anauzwa na aliombwa asaidie kushawishi klabu anayoitaka ifike kwetu na ofa yake. Ngasa alitamka bayana kuwa yupo tayari kwenda klabu yoyote ambayo Azam FC itaona imekidhi mahitaji yake kwa masharti kuwa maslahi yake ya kimkataba kati yake na Azam FC yazingatiwe.
2. Hadi kufikia siku ya Jumatano 01/08/2012 saa saba mchana. Ni klabu ya Simba pekee iliyojibu kwa maandishi na kuonesha nia ya kumchukua Ngasa. Yanga wao hawakuwahi kujibu email, ingawa kwa majibu ya simu Mjumbe wao wa Kamati ya usajili Bw Sefu Magari alitangaza kuwa Ngasa hana thamani ya zaidi ya milioni 20. Na Yanga haikuwa tayari kuboresha ofa yake.
3. Muda wa kufungwa kwa biashara ya kumuuza Ngasa ulipofika, ni simba pekee kupitia kwa makamu Mwenyekiti wake Bw Geofrey Ngange na Mhasibu wake ndiyo waliofika wakiwa na pesa taslimu shilingi milioni 25. Yanga hawakuonekana na hawakutaka kupokea hata simu walizokuwa wakipigiwa kuulizwa kama wana interest.
4. Kikao cha dharura cha Azam FC kilikaa na kuamua kuwa biashara ya kumuuza Ngasa ilishindikana kutokana na kutokupatikana kwa mnunuzi mwenye dola 50,000. Kwa maana hiyo Azam FC iliamua kumpeleka Ngasa kwa mkopo kwenye klabu iliyofika na kuonesha nia ya kumhitaji (Simba)
5. Simba walipewa sharti la kuhakikisha wanamlipa Ngasa mshahara wake kamili (TZsh 2,000,000) pamoja na stahiki zake nyingine zote za kimkataba
6. Sababu za kumpeleka Ngasa kwa mkopo ni kumuepusha na adhabu ambayo klabu ya Azam FC ingetoa kwa Ngasa kama angebaki.
7. Azam FC inapenda kuweka wazi kuwa haijamlazimisha Ngasa kwenda Simba kama inavyopotoshwa. Kama Ngasa anataka kuvunja mkataba wake au kama Yanga bado wanamhitaji basi waje na dola 50,000 na Azam FC itawauzia kwani licha ya kwamba amepelekwa kwa mkopo simba lakini Ngasa bado ni mali ya Azam FC
8. Tunaomba kuweka msimamo wetu kuwa hatupo tayari kumlipa Ngasa na kuvunja mkataba wake na hatuna sababu ya kufanya hivyo. Kama Ngasa hataki kwenda tunakompeleka Azam FC inamruhusu kubakia klabuni na kutumikia adhabu.
9. Lakini Ngasa na washauri wake waelewe kuwa akiamua kubaki Azam FC atakaa nje ya uwanja kwa muda wote uliosalia kwenye mkataba wake, kwani Azam FC haipotayari kumvisha jezi mchezaji anayefanya vitendo vya utovu wa nidhamu.
10. Kwa kuwa Sakata hili limeanza kuhusishwa na sakata la Mchezaji ramadhani Chombo. Naomba nitoe ufafanuzi kama ifuatavyo. Redondo alipewa option tatu za kuchagua baada ya kufanya vitendo vya utovu wa nidhamu timu ilipokuwa safarini Mwanza.
a. Kupelekwa kwa mkopo Moro United?
b. Kupatikana kwa mnunuzi mwenye shilingi milioni 40
c. Kukubali adhabu ya kufungiwa kwa miezi mitatu na kulipwa nusu mshahara wahati akitumikia adhabu.
Redondo alithibitisha kuipenda Azam FC kwa kukataa kuuzwa au kupelekwa kwa mkopo. Alikubali kutumikia adhabu yake na ilipoisha alirudi na kuomba msamaha na sasa ni mmoja kati ya wachezaji wenye nidhamu ya hali ya juu sana. Azam FC inajivunia kuwa na mchezaji kama Redondo na bila kupepesa macho wala kung’ata maneno. Azam FC inamchukulia Redondo kama mtu spesho na mwenye mapenzi ya dhati na klabu yake na inamtaka aendelee kuwa na moyo huo.
Imetolewa na utawala.
Azam FC
0 Maoni:
Post a Comment