BEKI wa pembeni wa Azam FC, Samih Hajji Nuhu ameondoka alfajiri ya leo kwenda Cape Town kupitia Johannesburg, Afrika Kusini kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji wa goti la mguu wa kushoto.
Nuhu ameongozana na Daktari Mkuu wa Azam FC, Dk Mwanandi Juma Mwankemwa pamoja na Mweka Hazina wa timu, Abdulkarim Shermohamed Bahadour maarufu kama Karim Mapesa.
Mzanzibari huyo atafanyiwa upasuaji katika hospitali ya Vincent Palocci mjini Cape Town na Mtaalamu, Dk. Nicholas, ambaye ameweza kuwarudisha uwanjani wachezaji wengi wa Afrika Kusini waliopata maumivu makubwa.
Hii itakuwa mara ya tatu kwa Nuhu kufanyiwa operesheni ya goti hilo, baada ya awali kufanyiwa mara mbili nchini India, kwanza katika hospitali ya Mumbai chini ya Dk. Tanna na ya pili hospitali ya Pune.
Nuhu amekuwa nje ya Uwanja tangu mwaka jana na msimu huu wote hajagusa mpira kwa sababu ya maumivu hayo. Ni matarajio ya uongozi wa timu kwamba tiba ya Afrika Kusini itamrejesha uwanjani mchezaji huyo kinda mwenye kipaji.
0 Maoni:
Post a Comment