Klabu ya Azam FC imemsajili kwa mkataba wa miaka
mitatu beki chipukizi wa kati, Abdallah Kheri Salum wa klabu ya Zimamoto
ya Zanzibar.
Beki huyo mwenye uwezo pia wa kucheza nafasi ya
kiungo, kwa sasa yupo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya vijana walio na
umri chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes.
Katibu mkuu wa Azam FC, Nasoro Idrisa, alisema:
“Ni mchezaji mdogo mwenye kipaji, ambaye wasaka vipaji wetu
wamejiridhisha kuwa atakuwa msaada kwa timu yetu baadaye. Hivyo tumeamua
kumpa mkataba wa miaka mitatu.”
Naye Salum alisema amefurahia kujiunga na ‘Wana
lambalamba’ hao kwa vile ni miongoni mwa timu kubwa na aliahidi kutumia
fursa hiyo kuendeleza kipaji chake.
“Azam ndiyo mabingwa wa Tanzania Bara. Ni timu
kubwa na bora ambayo naamini ni bahati kwangu kujiunga nayo. Ninaamini
nitaendeleza kipaji changu na kutimiza ndoto za kuwa mchezaji bora
baadaye,” alisema Salum.
Kinda huyo anakuwa mchezaji wa nne kusajiliwa na
Azam baada ya kumalizika kwa msimu huu na kutwaa taji la kwanza la
ubingwa wa Tanzania Bara.
Wengine walionaswa na Azam ni kiungo Frank Domayo
na mshambuliaji Didier Kavumbangu waliojiunga na timu hiyo wakitokea
Yanga, pamoja na mshambuliaji Ismaila Diara kutoka Mali.
Mkakati mwingine wa klabu hiyo ni kumsajili kiraka, Shomari Kapombe kutoka AS Cannes ya Ufaransa.
0 Maoni:
Post a Comment