Jean Baptiste Mugiranea ‘Migi’ ni kiungo mkabaji wa Azam FC aliyesajiliwa kutoka klabu ya APR FC ya Rwanda, baada ya kutua kwenye kikosi cha ‘waoka mikate’ wa jiji la Dar es Salaam aliisaidia timu hiyo kutwaa kombe la CECAFA Kagame Cup bila kupoteza mchezo hata mmoja huku wakiwa hawajaruhusu goli hata moja kwenye dakika 90 za mechi zote.
Mtandao huu umefanya mahojiano mafupi na Mnyarwanda huyo anaekipiga pia kwenye timu ya taifa ya Rwanda ‘The Amavubi’ ili kujua machache kuhusu maisha yake ya soka tangu ametua Azam FC na mwanzo wake kwenye ligi kuu Tanzania bara ambapo amecheza mechi yake ya kwanza ya VPL wakati Azam ilipocheza na Tanzania Prisons kwenye uwanja wa Azam Complex, Chamazi.
Shaffihdauda.com: Kunatofauti gani kati ya ligi ya Tanzania na ile ya nchini Rwanda ambayo wewe umetokea ukiwa unacheza kwenye klabu ya APR FC?
Migi: Nimeona tofauti kubwa sana kwenye ligi ya Vodacom ukilinganisha na ligi ya Rwanda, kila timu hapa inajituma hakuna timu ndogo, timu ndogo inakuja inapambana kama timu kubwa na inauwezo wa kupata pointi tatu kama ilivyokuwa kwenye mechi yetu ya kwanza dhidi ya Tanzania Prisons.
Shaffihdauda.com: Kikosi cha Azam kimesheheni wachezaji wengi wenye vipaji na uwezo wa hali ya juu, wewe ni mchezaji mpya vipi vita ya namba ikoje kwenye kikosi?
Migi: Mimi siwezi kusema kama nina nafasi kwenye kikosi cha Azam, wala sijaja hapa kugombea nafasi. Niekuja hapa kuleta experience yangu niunganishe na wenzangu niliowakuta hapa ili kuona kama mwaka huu tutachukua ubingwa.
Shaffihdauda.com: Unawaahidi nini mashabiki wa Azam na wapenda soka wote wa nchini Tanzania?
Migi: Nachoweza kuwaambia mashabiki wa Azam kuwa, tuna timu nzuri kama tuliweza kucheza mashindano ya Kagame bila kufungwa lakini wachezaji wengine wengi hawakuwepo. Kwasasa tumeungana timu nzima na naamini tutafanya vizuri, ila wachezaji kama tunafikiria kombe inabidi tujitume zaidi.
Shaffihdauda.com: Itakuwaje endapo kama kunatimu nyingine itataka kukusajili, au unadhani tayari umeshafika Azam?
Migi: Mimi nina mkataba na Azam na ni mchezaji halali wa Azam. Ninavitu vingi vya kuifanyia Azam, bado mgeni hapa naweza kusema bado najitafuta ili nikae vizuri kwenye ligi ya Tanzania bado ninavitu vingi vya kuwaonesha mashabiki Azam, wanipe muda tu niendelee kuzoea nadhani baada ya muda mambo yatakuwa mazuri.
Chanzo: shaffihdauda.co.tz
0 Maoni:
Post a Comment