TIMU ya Azam FC leo Jumamosi saa 2 asubuhi, itahamishia mazoezi ufukweni kwenye Fukwe za Bahari ya Coco jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujiweka fiti kuelekea mechi zake zijazo.
Azam FC inahamia ufukweni ikiwa ni siku nne tu tokea ianze mazoezi Jumanne iliyopita baada ya kumalizika kwa likizo ya wiki tatu kufuatia Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kusimama.
Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, anapendelea sana kuwanoa wachezaji wake ufukweni, ili kuwaweka fiti kimwili na kujenga misuli yao pamoja na kuwaongezea pumzi.
Meneja wa Azam FC, Luckson Kakolaki, ameiambia azamfc.co.tz kuwa mazoezi yanaendelea vizuri kwa wachezaji wote wa timu kubwa takribani 11 waliochanganyika na wa Azam Academy.
"Wachezaji wote wasiokuwa kwenye timu za Taifa wamewasili, wa kimataifa Kipre Tchetche, Michael Bolou nao wapo, wanafanya mazoezi pamoja na wachezaji wa academy," alisema.
Kakolaki alisema mchezaji pekee kigeni ambaye hajawasili nchini na hayumo kwenye timu ya Taifa ni beki Pascal Wawa, aliyeomba ruhusa maalum na atawasili nchini mwishoni mwa mwezi huu.
Wakati huo huo, beki wa kati Aggrey Morris, yeye bado anaendelea na matibabu chini ya uangalizi wa madaktari wa Azam FC baada ya kuripoti kambini akitokea timu ya Taifa ya Zanzibar 'Zanzibar Heroes' akiwa ameumia.
Nyota wa timu kubwa wa Azam FC wanaoshiriki michuano ya Kombe la Chalenji ni nahodha John Bocco 'Adebayor', Nahodha Msaidizi Himid Mao 'Ninja', kiungo Salum Abubakar 'Sure Boy', kipa Aishi Manula, beki Shomari Kapombe, wanaoing'arisha vema Kilimanjaro Stars iliyotinga Robo Fainali.
Wengine ni mshambuliaji Ame Ally, winga Khamis Mcha 'Vialli' na kiungo Mudathir Yahya 'Muda', walioko Zanzibar Heroes, huku mshambuliaji Allan Wanga akiwa na Kenya 'Harambee Stars' na kiungo Jean Baptiste Mugiraneza 'Migi' akipeperusha bendera ya Rwanda 'Amavubi'.
Azam FC inakabiliwa na mechi mbalimbali za ligi ikiwemo ijayo dhidi ya Simba, michuano ya Kombe la Mapinduzi, Kombe la FA na Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.
0 Maoni:
Post a Comment