UONGOZI wa timu ya Azam FC umekanusha taarifa zinazomhusisha mshambuliaji wake Kipre Tchetche kuondoka katika timu hiyo katika kipindi cha usajili wa dirisha dogo, unaofunguliwa Novemba 15, mwaka huu.
Hiyo inatokana na uvumi unaoendelea kuvumishwa kila siku kwenye vyombo vya habari, vikieleza kuwa tayari kuna timu za hapa nchini zimebisha hodi kwa uongozi wa Azam FC vikitaka kumsajili straika huyo hatari.
Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, aliuambia mtandao wa azamfc.co.tz kuwa, taarifa hizo si za kweli na mpaka sasa hawajapokea barua yoyote kutoka kwa timu zinazodaiwa kumtaka Tchetche.
“Hakuna barua yoyote tuliyopokea mpaka sasa kama inavyodaiwa, Kipre Tchetche bado ni mchezaji wetu na ana mkataba mrefu na ataendelea kuwa hapa na yeye ana furaha kubwa kuwa hapa,” alisema.
Kawemba aliongeza kuwa; “Kwa sasa wachezaji wetu wote wapo mapumzikoni, hivyo mimi nigependa kuziomba klabu ziache kuwasumbua wachezaji wetu katika kipindi hiki wakiwa wamepumzika.”
Uongozi wa Azam FC pia umewataka mashabiki wa timu hiyo kuwa watulivu katika kipindi hiki cha usajili, na taarifa zozote za kuuzwa mchezaji au kununuliwa, zitatolewa na vyanzo rasmi vya habari vya klabu.
Tchetche, amekuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya Azam FC tokea mwaka 2011 alipojiunga nayo akitokea Jeunesse Club d'Abidjan Treichville (JCAT) ya Ivory Coast, ameiongoza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu wa 2013/14 na Kombe la Kagame mwaka huu, mataji waliyotwaa bila kufungwa mchezo hata mmoja.
Straika huyo mwenye kasi kubwa uwanjani, uwezo wa kupiga mashuti ya mbali na kupiga chenga za maudhi, pia amezoa tuzo binafsi uwanjani, akitwaa Uchezaji Bora wa ligi msimu wa 2013/14 na Tuzo ya Ufungaji Bora msimu wa 2012/13 kwa mabao 17 aliyofunga.
Wakati Azam FC ikiwa kileleni kwa pointi 25 msimu huu baada ya kushinda mechi nane na sare moja, Tchetche amefunga jumla ya mabao sita mpaka sasa ndani ya mechi tisa, akizidiwa mabao matatu na aneyeongoza kwenye msimamo, Elias Maguli, aliyefunga tisa.
Kipre Tchetche hang’oki Azam FCUONGOZI wa timu ya Azam FC umekanusha taarifa zinazomhusisha mshambuliaji wake Kipre...
Posted by Azam FC on Tuesday, November 10, 2015
0 Maoni:
Post a Comment