TIMU ya vijana ya Azam FC, mchana wa leo imewachapa vijana wenzao wa Simba mabao 2-1 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mchezo huo ulikuwa ni mahususi kwa ajili ya utangulizi wa mechi ya timu kubwa za klabu hizo kama sheria za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara zinavyoeleza.
Vijana hao wa Azam FC, walionekana kutakata sana kwenye mchezo huo, hasa kiungo wake mahiri Abdallah Masoud ‘Cabaye’, aliyekuwa akiwapeleka atakavyo wachezaji wa Simba kila alipogusa mpira.
Alikuwa ni kiungo Rajabu Odasi, aliyeipatia bao la uongozi Azam FC kwa shuti kali baada ya kuupokea mpira uliozuiwa na wachezaji wa Simba wakati alipopiga mpira wa adhabu ndogo.
Bao hilo lilidumu hadi kipindi cha kwanza kinamalizika na Simba ikafanikisha kupata la kusawazisha kipindi cha pili mwanzoni baada ya kutokea uzembe kwenye eneo la ulinzi.
Beki Abbas Kapombe ambaye ndiye nahodha wa kikosi hicho, aliihakikishia ushindi Azam FC Academy baada ya kupiga bao la pili kwa njia ya mkwaju wa penalti, iliyotokana na beki mmoja wa Simba kuunawa mpira wakati akiokoa krosi.
Kocha Mkuu wa Azam Academy, Tom Legg, aliyekuwa jukwaani kwenye mchezo wa leo, alitumia mechi hiyo kama sehemu ya kuwafanyia tathimini wachezaji wake baada ya kukosa mechi za kirafiki tokea alipoanza majukumu hayo mwanzoni mwa mwezi huu.
Wakati Legg, 28, akiwa jukwaani akiwasoma wachezaji wake pamoja na kuwafanyia tathimini hiyo, majukumu mengine yote alimwachia kocha wake msaidizi, Idd Cheche.
0 Maoni:
Post a Comment