WACHEZAJI wa timu ya Azam FC wameendelea na mazoezi ya nguvu kujiwinda na mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Simba keshokutwa Jumamosi huku wakiwa na morali ya hali ya juu ya kuifunga timu hiyo.
Azam FC imejipanga kufanya vizuri kwenye mchezo huo, ili kuendeleza mwenendo mzuri walioanza nao katika ligi pamoja na kutawala kileleni mwa msimamo, hivi sasa wakijikusanyia jumla ya pointi 25.
Jambo zuri la kuvutia kwenye mazoezi ya leo, imeshuhudiwa kiungo Mnyarwanda Jean Baptiste Mugiraneza ‘Migi’, akianza mazoezi yake ya kwanza baada ya kurejea nchini jana usiku akitokea nchini Ethiopia.
Benchi la Ufundi la Azam FC chini ya Kocha Mkuu Stewart Hall, Wasaidizi wake Mario Marinica na Dennis Kitambi, waliendelea kuwapa mazoezi ya mbinu wachezaji ikiwa ni sehemu ya kuwaweka fiti kwa ajili ya mchezo huo na mingine iliyo mbele yao.
Wachezaji waliokuwa na majeraha madogo, mabeki Aggrey Morris na David Mwantika, nao afya zao zimeonekana kuimarika na tokea juzi jioni wamekuwa ni sehemu ya nyota wa Azam FC wanaojiandaa vilivyo na mchezo huo.
Akizungumza na mtandao wa azamfc.co.tz, mara baada ya mazoezi ya leo, Kocha Mkuu Stewart Hall, alisema amefurahishwa na namna wachezaji wake walivyokuwa na morali kubwa kuelekea mchezo huo.
“Mazoezi yanaendelea vizuri, wachezaji morali zao zipo juu, wanaonyesha ushindani mazoezini jambo ambalo ni zuri, kila mmoja anaonyesha anataka kucheza mechi dhidi ya Simba, hata majeruhi Aggrey Morris na David (Mwantika), nao afya zao zinaimarika kila siku, hii inatuonyesha ishara nzuri benchi la ufundi,” alisema.
Kocha huyo wa zamani wa timu ya Taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’ na Sofapaka ya Kenya, alisema amepata furaha kuona Migi amerejea kikosini na kudai kuwa atamwangalia zaidi kwenye mazoezi ya leo jioni na kesho ili kujua kama atakuwa fiti kuelekea mchezo huo.
Hall aliongeza kuwa: “Kila siku mambo yanabadilika, lazima tushinde mchezo wa Jumamosi, hatuna chaguo jingine ikizingatiwa tuko kileleni na tunatakiwa kuendelea kuipigania nafasi yetu hiyo.”
Azam FC imekuwa na kikosi imara sana msimu huu chenye ushindani mkubwa wa namba hasa eneo la kiungo, akizungumzia hilo, Hall alisema kuwa kuna baadhi ya viungo amepanga kuwatumia kwenye mchezo huo na baadhi katika mchezo mwingine watakaocheza dhidi ya Majimaji Desemba 20, mwaka huu mkoani Songea.
“Viungo watakaocheza mchezo wa Simba watakuwa ni tofauti na wale wa mchezo wa Majimaji, tumejipanga kwa hilo kutokana na mazingira ya uwanja. Uwanja wa Taifa ni mzuri sana na ule wa Majimaji ni mbaya sana,” alisema Hall.
0 Maoni:
Post a Comment