BEKI kisiki wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, Aggrey Morris, anatarajia kuondoka nchini leo Jumanne saa 9.15 Alasiri na kuelekea nchini Afrika Kusini kufanyiwa matibabu ya nyuzinyuzi (ligaments) zinazounganisha mifupa ya goti lake la kulia.
Akizungumza na mtandao wa azamfc.co.tz, Daktari wa Azam FC, Juma Mwimbe, ambaye ataambatana na beki huyo nchini humo, alisema matibabu yote ya Morris yatafanyika katika Hospitali ya Afrisurb iliyopo jijini Cape Town, Afrika Kusini.
“Tutaondoka leo saa 9.15 alasiri na tutafika kule majira ya saa 4 usiku, kesho tutakwenda kwenye hospitali hiyo ili Morris akafanyiwe uchunguzi baada ya hapo kama vipimo vitaonyesha anatakiwa kufanyiwa upasuaji basi atafanyiwa, lakini ataanza kwanza na uchunguzi,” alisema kwa ufupi Dk. Mwimbe
Morris amekuwa mchezaji muhimu sana kwenye eneo la ulinzi la Azam FC akitengeneza kombinesheni nzuri na Muivory Coast, Pascal Wawa, kukosekana kwake kumemlazimu Kocha Mkuu Stewart Hall, amtumie kinda Abdallah Kheri ‘Sebo’, ambaye ameonekana kufanya vema mpaka sasa.
Mpaka sasa mechi za Azam FC alizozikosa Morris ni zile za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Simba, Majimaji, Kagera Sugar na Mtibwa Sugar, pamoja na michezo mitatu ya Kombe la Mapinduzi waliyochuana na Mtibwa Sugar, Yanga na Mafunzo.
0 Maoni:
Post a Comment