KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, Stewart Hall, ameelezea kiufundi kilichotokea kwenye mchezo wa jana wa michuano ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya Yanga huku akidai kuwa mwamuzi msaidizi namba mbili aliwapa wapinzani wao bao la kusawazisha lisilokuwa halali.
Mchezo huo wa Kundi ulishuhudiwa ukimalizika kwa timu hizo kutoka sare ya bao 1-1, Azam FC ilitangulia kupata bao la uongozi kupitia kwa Kipre Tchetche dakika ya 58 kabla ya Yanga kusawasisha kupitia kwa Vincent Bossou.
Akizungumza na mtandao wa azamfc.co.tz, mara baada ya mazoezi ya leo asubuhi yaliyofanyika Uwanja wa Fuoni, visiwani hapa Zanzibar, Hall alisema mchezo wao dhidi ya Yanga siku zote ni wa nguvu mno, hivyo walipaswa kupatikana waamuzi bora na sio waliochezesha mechi ya jana, ambao waliboronga mno.
"Nimefurahishwa na moyo na ufanyaji kazi wa bidii wa timu yangu kwa kiasi kikubwa licha ya mambo tuliyofanyiwa, tulianza mchezo kwa sisi basi letu kuzuiwa na tulinyimwa kuingia uwanjani kwa wakati, hili lilitufanya kupoteza dakika 20 za muda wetu wa maandalizi ya mchezo, hivyo hatukujiandaa vya kutosha na kupoteza muda wa kupasha moto mwili.
"Hii ilitusumbua sana na hatukuanza vizuri mchezo kwa sababu ya hilo, kwani tulifanya maandalizi ya haraka haraka na hatukutulia na Yanga yenyewe ilianza vizuri na kwa kiwango cha juu, lakini baada ya dakika 15 na 20 tulitulia na kucheza vizuri, lakini tatizo kubwa jingine ni waamuzi tulipewa kadi tatu za njano kipindi cha kwanza na Yanga hawakupewa na mechi ilikuwa ya kutumia nguvu ndio, unajua haikuwa ya kutumia nguvu kwa upande mmoja bali ni kwa pande zote mbili,” alisema.
Hall alisema kwa hali hiyo huwezi ukatoa kadi za njano kwa Azam FC na ukashindwa kuwapa Yanga huku akidai kuwa baada ya mapumziko walijua kuwa watamaliza mchezo huo wakiwa na wachezaji kumi uwanjani kutokana na mipango ya waamuzi.
"Kipindi cha pili tulirejea na kiwango cha juu na tulicheza vizuri na tukafunga bao, halafu kwa mara nyingine mwamuzi wakawa sababu kubwa, unajua kwanini Ngoma (Donald) amemsukuma Mudathir (Yahya) chini na kumpiga na hakupewa kadi yoyote hata ya njano, lakini Bocco (John) alipewa nyekundu, Bocco alitakiwa kupewa kadi nyekundu kwa alilofanya, lakini Ngoma ndiye aliyeanza tukio lile na tatizo yeye hakupewa kadi yoyote, hii ni aibu," alisema.
Alisema tatizo kubwa lilikuwa ni kutakiwa kucheza pungufu, lakini bao lao alikuwa halali kwani mpira haukuvuka mstari wa lango.
"Mwamuzi msaidizi (namba mbili) alikuwa usawa wa mstari wa eneo la penalti, aliwezaje kuona mstari wa lango wakati hakuwa kwenye eneo hilo na hakuweza kunyoosha kibendera juu na alisubiri, na baada ya mashabiki kuanza kupiga kelele, alinyanyua kibendera juu, kwa mara nyingine waamuzi wanasikitisha sana," alisema
Mwingereza huyo alisema kiukweli ingekuwa ni mimi ningeirudisha timu nyumbani na tusingecheza tena michuano ya Kombe la Mapinduzi.
"Nadhani michuano hii ni ya aibu sana na waamuzi wanatia aibu, ningeirudisha timu nyumbani, hawaangalii muda unaopoteza kwenye mazoezi na vikao vya timu, kama watu wanadanganya kuna tatizo na watu wanadanganya dhidi ya Azam, hivyo kwa mimi ningeirudisha timu nyumbani, sio maamuzi yangu, bodi ya wakurugenzi ndio inayoamua tucheze na sisi tunacheza hakuna tatizo," alisema.
Kwa mujibu wa takwimu za mchezo huo, zimeonyesha kuwa Yanga iliyofanya faulo 17 iliweza kupewa kadi moja tu ambayo ni ya njano, lakini Azam FC iliyofanya 14, ilionyeshwa kadi sita, za njano zikiwa tano na moja ikiwa nyekundu.
Mipango mechi ya kesho na Mafunzo
Kuelekea mchezo wao wa kesho wa mwisho wa makundi dhidi ya Mafunzo, Hall amesema wana malengo mawili makubwa, kuhakikisha wanashinda na kupata ushindi mnono wa kuanzia mabao mawili au matatu ili kusonga mbele kwa hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo.
"Jambo la kwanza tunatakiwa kushinda mechi, jambo la pili ni kushinda vizuri na tunataka kushinda mabao mawili au matatu bila kuruhusu bao na hapo tutafuzu vizuti bila tatizo," alisema.
Azam FC mpaka hivi sasa imefikisha pointi mbili katika nafasi ya tatu kufuatia sare mbili dhidi ya Mtibwa Sugar na Yanga, ambazo zipo juu yake zote zikiwa na pointi nne huku Mafunzo ikiwa imeshaaga michuano hiyo baada ya kutoambulia pointi yoyote mpaka sasa.
0 Maoni:
Post a Comment