Saturday, February 6, 2016

HALL AWAPIGIA HESABU MWADUI FC KESHO

Posted By: kj - 6:18 PM

Share

& Comment


KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, Stewart Hall amesema kuwa pointi tatu ndio kitu muhimu alichokidhamiria katika mchezo wa kesho wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Mwadui ya Shinyanga, utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex saa 10.00 jioni.

Azam FC itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na morali kubwa, hasa baada ya kutwaa ubingwa wa michuano maalumu ya timu nne iliyomalizika jijini Ndola Zambia Jumatano iliyopita.

Akizungumza na mtandao wa www.azamfc.co.tz mara baada ya mazoezi ya leo asubuhi, Hall alisema anajua kuwa mchezo huo utakuwa mgumu lakini amejipanga kukabiliana na presha zote za ndani ya nje ya uwanja na kupata ushindi.

“Mchezo wa kesho ni mkubwa, kwa sababu tulikuwa na mapumziko ya mechi zetu za ligi, tulicheza mchezo wa Kombe la FA, tukaenda Zambia tukacheza mechi tatu, hivyo tumecheza mechi nne tukiwa katika mapumziko hayo, hivyo kwa kesho kitu muhimu kesho ni pointi tatu,” alisema.

Kocha huyo wa zamani wa Zanzibar Heroes, Sofapaka ya Kenya na Academy ya Birmingham City, alisema kuwa anategemea ugumu kwenye mchezo kama aliokutana nao katika mechi yao ya kwanza waliocheza Uwanja wa Mwadui na kuisha kwa kuibuka kidedea kwa ushindi wa bao 1-0.

“Unajua baadhi ya wapinzani wetu kwenye vita ya ubingwa sasa hivi wamelala, hivyo tunatakiwa kutumia mwanya huo sisi kufanya vizuri kwa kuanza kushinda kesho, najua kutakuwa na vita kubwa lakini tumejipanga kwa hilo,” alisema.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB, bado itaendelea kuwakosa baadhi ya nyota wake kama vile, mabeki Aggrey Morris, Racine Diouf na mshambuliaji Didier Kavumbagu, huku winga Farid Mussa akiwa na hatihati baada ya kupata majeraha madogo ya kisigino wakati timu ikiwa Zambia, lakini kesho atafanyiwa mazoezi ya utimamu wa kimwili kujua kama atakuwa fiti kucheza mchezo huo.

Azam FC itaingia kwenye mchezo huo ikiwa inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi kwa kujikusanyia jumla ya pointi 39 sawa na Simba iliyo juu yake huku Yanga ikiwa kileleni kwa pointi 40.

Lakini Yanga na Simba zote zimeizidi Azam FC michezo miwili, hivyo kwa vyovyote vile ikishinda mechi zake hizo za viporo pamoja na nyingine itapanda moja kwa moja kileleni katika msimamo wa ligi.

Mwadui yenyewe inakamata nafasi ya tano kwenye msimamo ikiwa na pointi 28 baada ya kushinda mechi nane, sare nne na kufungwa mara tano, ambapo mchezo wake wa mwisho ilifungwa bao 1-0 na African Sports ya Tanga.

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.