Sunday, February 21, 2016

HALL: TULICHEZA VYEMA NA MESSI ALIKUWA MCHEZAJI BORA HAPO JANA

Posted By: kj - 6:29 PM

Share

& Comment


BENCHI la Ufundi la Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, limefurahishwa na kiwango cha timu hiyo walichokionyesha katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Mbeya City, uliofanyika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya jana.

Kiwango hiko bora kiliifanya Azam FC kupata ushindi wa pili mnono kwenye ligi msimu huu kwa mechi za ugenini baada ya kuichapa Mbeya City mabao 3-0, ushindi wa kwanza mkubwa ugenini ulikuwa dhidi ya JKT Ruvu (4-2), uliofanyika Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.

Mabao ya Azam FC jana yalifungwa na Kipre Tchetche dakika ya 41, nahodha John Bocco ‘Adebayor’ (dk 63) na Farid Mussa aliyeingia kipindi cha pili akishindilia msumari wa mwisho dakika ya 84.

Akizungumza na mtandao wa www.azamfc.co.tz Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, alisema kuwa jana walionyesha kiwango safi baada ya kufanyia kazi udhaifu uliojitokeza katika mchezo uliopita dhidi ya Coastal Union kwa kushindwa kuutendea haki mfumo wa 3-5-2 wanaoutumia.

“Tulijitahidi kufanya mazoezi kuondoa kiwango cha chini haraka iwezekanavyo katika mfumo wetu na nadhani leo kiwango chetu kilikuwa cha hali ya juu. Tulianza kwa hali ya chini, tulionekana hali yetu ya kujiamini ilikuwa chini dakika 10 hadi 15 za kipindi cha kwanza na hii ilitokana na matokeo tuliyopata wiki iliyopita (Coastal Union).

“Lakini baada ya hapo tulianza kujenga vema kiwango chetu na nadhani kipindi cha pili tulikuwa vizuri zaidi, tulifanya mabadiliko ya kimbinu kipindi cha pili, tulimpeleka Messi (Ramadhan Singano) katikati na kumchezesha Farid (Mussa) upande wa kushoto aliyeingia kuchukua nafasi ya Mudathir Yahya,” alisema.

Hall alisema walifanya mabadiliko ya kumtoa Mudathir ili kuiongezea ubora timu eneo la katikati baada ya kipindi cha kwanza kukosa mtu wa kuwaunganisha vema wachezaji na kubakia kucheza sana mipira mirefu.

“Messi alikuwa mzuri sana katikati na ndiye mchezaji wetu bora katika kipindi cha pili, tulicheza sana mipira mirefu kipindi cha kwanza na kukosa mtu wa kuwaunganisha wachezaji, alipingia Messi katikati aliweza kutekeleza vizuri jambo hilo na kuanza kucheza mpira safi na nimefurahia hali ya leo (jana) sisi kutoruhusu bao kwani ni jambo zuri,” alisema.

Mwingereza huyo aliongeza kuwa siku zote hawaamini waamuzi na ndio jambo kubwa lililomfanya ampumzishe takribani dakika 25 za mwisho Nahodha Msaidizi Himid Mao na kuingia Frank Domayo, ikiwa ni baada ya kiungo huyo bora mkabaji kuonyeshwa kadi ya njano kipindi cha kwanza.

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.