Nahodha wa Azam FC John Raphael Bocco akijaribu kumtoka mlinzi wa Bidvest Wits |
Azam FC ikicheza kwa kiwango bora kabisa kwenye mchezo huo wa raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika uliofanyika Uwanja wa Bidvest Wits jijini Johannesburg, iliweza kuwachapa wenyeji wao hao mabao 3-0.
Katika mtanange huo uliokuwa mkali muda wote ulimshuhudia beki kisiki wa kati Aggrey Morris akirejea kwa mara ya kwanza kikosini baada ya kutoka kuuguza majeraha ya goti aliyopata Novemba mwaka jana alipokuwa na kikosi cha timu ya Taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’.
Mabingwa hao wa Kombe la Kagame walianza vema mchezo huo kwa kufanya shambulizi kali langoni mwa Bidvest baada ya Sure Boy kuwalamba chenga wachezaji wao wawili lakini pasi ya mwisho aliyopiga nje kidogo ya eneo la 18 iliweza kuokolewa vema na mabeki.
Sehemu ya kiungo ya Azam FC ambayo leo iliundwa na Himid Mao ‘Ninja’, Michael Bolou na Sure Boy na kipindi cha pili alipoingia Frank Domayo (akitoka Bolou) ilifanya kazi kubwa kwenye mchezo wa leo kwa kuidhibiti vilivyo Bidvest Wits iliyokuwa ikitumia mashambulizi ya pembeni na mipira mirefu.
Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika timu zote ziliweza kwenda vyumbani zikiwa suluhu, ambapo kipindi cha pili kilianza kwa Azam FC kuendeleza kasi yao ya kupeleka mashambulizi langoni mwa Bidvest Wits.
Juhudi hizo zilizaa matunda dakika ya 51 baada ya kaundika bao la uongozi kupitia kwa Sure Boy aliyepiga shuti nje ya eneo la 18 lililowapenya mabeki kadhaa wa Wits na mpira kujaa wavuni.
Sure Boy alipata nafasi hiyo ya kupiga shuti baada ya kona aliyochonga Ramadhan Singano ‘Messi’ kuokolewa vibaya na mabeki wa Wits na kukutana na mpira huo alioupeleka moja kwa moja wavuni.
Azam FC iliendeleza kasi yao kwa washambuliaji Bocco na Didier Kavumbagu kuwasumbua vilivyo mabeki wa Wits ambao walionekana kuzidiwa na kasi ya mchezo.
Hali hiyo iliipa mwanya Azam FC kuandika bao la pili dakika ya 56 kufuatia uzembe wa mabeki wa Wits walimrudishia vibaya mpira kipa wao, hali iliyomfanya Kapombe kukimbia kwa kasi na kuserereka na mpira huo uliopishana na kipa aliyekuwa ameutokea na kujaa wavuni.
Hilo ni bao la tisa la Kapombe msimu huu kwenye mashindano yote aliyoshiriki akiwa kama beki mwenye majukumu pia ya kushambulia kama winga (wing back).
Azam FC ilizidi kuendeleza kasi yake ya kusaka ushindi mnono ugenini na jitihada hizo zilizaa matunda dakika ya tatu baadaye baada ya nahodha Bocco kufunga bao la tatu kufuatia pasi safi ya Kavumbagu.
Mabingwa hao walipata sapoti kubwa leo ya mashabiki takribani 200 waliokuwa wakiishangilia kwa nguvu muda wote wa mchezo na kuwanyamazisha mashabiki wa Bidvest Wits.
Jambo kubwa jingine kikosi hicho leo kilipata bahati ya kuangaliwa jukwaani na mabosi wa timu hiyo Aboubakar Bakhressa, Omary Bakhressa na Jamal Bakhressa waliokuwa pamoja na viongozi wa timu hiyo Ofisa Mtendaji Mkuu Saad Kawemba, Makamu Mwenyekiti Nassor Idrissa.
Ushindi huo umeivuruga Bidvest Wits ambayo inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Afrika Kusini na hadi mchezo huo unamalizika walinywea na kutoamini kilichotokea kwenye uwanja wao wa nyumbani.
Azam FC inatarajia kurudiana na Bidvest Wits wiki moja ijayo (Machi 20) kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam huku ikitakiwa kupata ushindi wowote ama sare kuweza kusonga mbele kwa raundi ya pili.
Kikosi hicho kitaondoka kesho saa 9 mchana jijini hapa Johannesburg kwa saa za Afrika Mashariki tayari kabisa kurejea jijini Dar es Salaam kwa maandalizi ya mchezo wa marudiano na ule wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Stand United utakaofanyika Jumatano ijayo (Machi 16) kwenye Uwanja wa Azam Complex.
Azam FC leo: Aishi Manula, Shomari Kapombe/Waziri Salum, Aggrey Morice, Pascal Wawa, Erasto Nyoni, Michael Bolue/Franky Domayo, Himid Mao, Salum Abubakari, John Bocco na Dider Kavumbagu/Hamisi Mcha.
0 Maoni:
Post a Comment