Hiyo ni sare ya pili mfululizo kwa timu zote mbili baada ya mechi zao zilizopita kutoka tena sare, Azam FC ikitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Toto Africans huku Ndanda ikiambulia suluhu walipokipiga na Tanzania Prisons.
Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB, ndio ilikuwa ya kwanza kuziona nyavu za Ndanda baada ya Ramadhan Singano ‘Messi’ kupiga shuti kali dakika ya 16 akimalizia pasi nzuri aliyopewa na Michael Bolou.
Didier Kavumbagu aliiongezea Azam FC bao la pili dakika ya 42 kwa shuti kali la juu baada ya kuwazidi ujanja mabeki wa Ndanda waliozembea kuukoa mpira uliotemwa vibaya na kipa wao, Jeremia Kisubi kufuatia shuti alilopigiwa na Wazir Salum.
Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, Azam FC iliondoka kifua mbele kwa mabao hayo na ilikianza kipindi cha pili kwa kufanya mabadiliko ya kumtoa beki Racine Diouf, aliyepata kadi ya njano baada kumfanyia madhambi Atupele Green, nafasi yake ilichukuliwa na David Mwantika, pia alitoka Wazir na kuingia Mudathir Yahya.
Ndanda ilionekana kucheza vizuri zaidi kipindi cha pili na kufanikiwa kupata mabao mawili ya kusawazisha, la kwanza wakifunga dakika ya 52 kwa mkwaju wa penalti kupitia kwa Atupele hii ni baada ya kipa Aishi Manula kumfanyia madhambi Paul Ngalema.
Bao jingine lilifungwa dakika mbili za mwisho na Ahmed Msumi, akitumia vema uzembe wa safu ya ulinzi ya Azam FC na hivyo kufanya mpira huo kumalizika kwa sare hiyo.
Lakini katika hali isiyokuwa ya kawaida dakika ya 72 mwamuzi wa mchezo huo Ahmada Simba kutoka Kagera, alishindwa kuipa Azam FC pigo la penalti baada ya Kipre Tchetche kushikwa na kuvutwa jezi ndani ya eneo la 18 na mabeki wa Ndanda akiwa anatazamana na kipa hadi kupelekea kudondoka chini huku mwamuzi huyo akishuhudia.
Hivyo kwa matokeo hayo Azam FC imefikisha jumla ya pointi 52 na kubakia katika nafasi ya tatu huku ikizidiwa pointi moja na Yanga inayoshika nafasi ya pili na pointi tano dhidi ya Simba iliyo kileleni, lakini imeizidi Yanga mchezo mmoja huku ikizidiwa mechi moja na Wekundu hao.
Mara baada ya mchezo huo kikosi cha Azam FC kimeendelea kubakia kambini kwa ajili ya maandalizi ya mchezo ujao wa raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Esperance de Tunis ya Tunisia utakaofanyika Jumapili ijayo (Aprili 10) kwenye Uwanja wa Azam Compex.
0 Maoni:
Post a Comment