Monday, May 23, 2016

AZAM FC YAMALIZA YAPILI

Posted By: Unknown - 12:02 PM

Share

& Comment

KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, leo jioni imemaliza katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Mgambo JKT ya Tanga.

Mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Azam Complex ulikuwa ni wa kuhitimisha pazia la ligi hiyo msimu huu, Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB imefikisha jumla ya pointi 64 na kuimaliza Simba iliyokuwa ikiwania nafasi hiyo ambayo leo imefungwa 2-1 na JKT Ruvu na kubakia na pointi zake 62.

Matokeo hayo ya sare yameifanya Mgambo JKT kushuka rasmi daraja baada ya kujikusanyia pointi 28 na kuungana na timu nyingine mbili za Tanga, African Sports (26) na Coastal Union (22) ambazo nazo zimeshuka daraja.

Kwa mara ya kwanza kwenye mchezo huo msimu huu benchi la ufundi la Azam FC liliongozwa na makocha wazawa, Kocha Mkuu wa muda hadi kumalizika kwa msimu huu, Dennis Kitambi na Msaidizi wake Idd Cheche, na hii ni kutokana na kuachia ngazi kwa Kocha wa zamani wa timu hiyo Stewart Hall aliyeondoka na benchi lake zima la ufundi isipokuwa Kitambi aliyebakia.

Azam FC katika mchezo huo ilionyesha uhai mkubwa hasa kipindi cha kwanza ikicheza soka la kasi na pasi fupi fupi, lakini umakini mdogo wa safu ya ushambuliaji uliwanyima mabao mengi katika vipindi vyote viwili hasa Kipre Tchetche aliyekosa takribani nafasi tano za wazi.

Ubora wa soka la leo la Azam FC unatokana na mafunzo waliyoanza kupewa na makocha wapya kutoka Hispania, Kocha Mkuu Zeben Hernandez na Jonas Garcia, ambaye ni Mtaalamu wa mazoezi ya viungo, ambao walishuhudia mchezo huo jukwaani.

Bao la Azam FC lilifungwa kiufundi na winga Ramadhan Singano ‘Messi’ dakika ya 60 kwa shuti kali akimalizia kazi nzuri iliyofanywa na Mudathir Yahya, ambaye kiwango chake kilionekana kuimarika leo tofauti na mechi nyingine alizocheza msimu huu.

Mgambo JKT ilioenekana kucharuka kipindi cha pili hasa baada ya kufungwa bao hilo na hatimaye dakika ya 71 ikapata penalti kufuatia beki wa Azam FC, David Mwantika, kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari, ambayo ilifungwa vema na kiungo Ally Nassoro Ufudu dakika moja baadaye.

Ukosefu wa umakini wa Tchetche na Allan Wanga, uliinyima Azam FC mabao ya kufunga dakika za mwisho za kipindi hicho na hatimaye dakika 90 zikamalizika kwa timu zote kugawana pointi moja moja.

Mara baada ya mchezo huo kumalizika wachezaji wa Mgambo JKT waliinama chini na kulala uwanjani wengine wakilia kama vile mshambuliaji wao Mohamed Samatta, hasa kutokana na kushuka daraja baada ya misimu minne waliyodumu Ligi Kuu tokea wapande kwa mara ya kwanza msimu wa 2012/13.

Azam FC kutwaa nafasi hiyo ya pili inatarajiwa kupokea zawadi ya Sh. milioni 40 kutoka kwa wadhamini wa ligi Kampuni ya Vodacom, nusu ya fedha itakayopokea Yanga iliyoibuka mabingwa msimu huu kwa kutetea ubingwa wao.

Hadi ligi hiyo inahitimika mfungaji bora amefanikiwa kuwa mshambuliaji wa Yanga, Amissi Tambwe, aliyefunga mabao 21 msimu huu na kuandika rekodi ya kutwaa kiatu hicho mara mbili, mara ya kwanza akikibeba wakati akiwa Simba msimu 2013/14 Azam FC ilipokuwa mabingwa, ambapo alipopachika wavuni mabao 19.

Kikosi Azam FC:
Aishi Manula, Wazir Salum/Gadiel Michael dk 46, Erasto Nyoni, Aggrey Morris, David Mwantika, Michael Bolou, Mudathir Yahya/Ame Ally dk 80, Salum Abubakar, Himid Mao (C), Kipre Tchetche, Ramadhan Singano/Allan Wanga dk 65

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.