Thursday, May 26, 2016

Fainali FA Cup: Azam FC yapoteza, Aishi kipa bora

Posted By: kj - 12:43 PM

Share

& Comment

KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, imeshindwa kutwaa ubingwa wa michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) baada ya jana kufungwa na Yanga mabao 3-1.

Azam FC iliingia kwenye fainali hiyo ikiwa inataka kuandika rekodi ya kuchukua taji hilo kwa mara ya kwanza huku pia ikitaka kumaliza msimu na rekodi ya aina yake ya kutwaa mataji mawili baada ya Agosti mwaka jana kubeba taji la Kombe la Kagame.

Timu hiyo inayodhaminiwa na Benki ya NMB ilianza mchezo huo kwa kasi na kufanya shambulizi kali langoni mwa Yanga, lakini shuti lililopigwa na Farid Mussa kufuatia pasi safi ya Mudathir Yahya lilidakwa vema na kipa wa Yanga, Deogratius Munishi ‘Dida’.

Yanga iliamka na kufanya mashambulizi kadhaa langoni mwa wapinzani wao na kufanikiwa kupata bao la uongozi dakika ya tisa lililofungwa kwa kichwa na mshambuliaji Amissi Tambwe akimalizia krosi iliyochongwa na Juma Abdul.

Azam FC ingekuwa makini ingeweza kupata mabao mawili katika dakika ya 24 na 35, lakini wachezaji wake kiungo Mudathir Yahya na nahodha John Bocco ‘Adebayor’, walikosa umakini na kupoteza nafasi hizo na hivyo kufanya Yanga imalize kipindi cha kwanza ikiwa kifua mbele kwa bao hilo.

Kipindi cha pili kilianza kwa Azam FC kufanya mabadiliko katika safu ya ushambuliaji akitoka Bocco aliyepata majeraha ya mguu na nafasi yake kuchukuliwa na Didier Kavumbagu.

Wanajangwani hao waliendeleza kasi yao kipindi cha pili na kupata bao la pili dakika ya 47 lililofungwa na Tambwe tena kwa shuti akiunganisha pasi aliyopigiwa na Simon Msuva.

Kavumbagu aliweza kuirudisha mchezoni Azam FC dakika moja baadaye baada ya kuifungia bao hilo la kufuatia machozi kwa kifua akiunganisha krosi safi aliyopigiwa na Ramadhan Singano ‘Messi’.

Wakati Azam FC ikifanya jitihada za kutafuta bao la kusawazisha ilijikuta ikifanya makosa kwenye ukabaji na kuwaruhusu Yanga kuandika bao la tatu dakika ya 81 lililofungwa na winga Deus Kaseke na hivyo kufanya dakika 90 za mchezo huo uliochezeshwa na mwamuzi Israel Nkongo, kumalizika kwa ushindi wa timu hiyo.

Azam FC kutwaa nafasi hiyo ya pili kumewafanya kujizolea medali za shaba za ushindi wa pili huku Yanga ikitwaa kikombe cha ubingwa, medali za dhahabu na kiasi cha fedha chenye thamani ya Sh. milioni 50.

Licha ya Yanga kutwaa ubingwa huo, Azam FC tayari imefanikiwa kukata tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika mwakani huku Yanga ikiwakilisha kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kutwaa taji la ligi.

Aishi Manula ang’ara

Kipa wa Azam FC Aishi Manula, aliyefanya jitihada kubwa sana kwenye mchezo huo kwa kuokoa michomo hatari ya wachezaji wa Yanga, amefanikiwa kutamba kwenye tuzo binafsi za wachezaji waliofanya vizuri katika michuano hiyo.

Aishi amefanikiwa kuwa Kipa Bora wa FA Cup na kujibebea tuzo maalumu ya kumpongeza kwa kazi kubwa aliyofanya tokea mwanzo hadi mwisho wa michuano hiyo, ambayo ilishirikisha timu za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), Daraja la Kwanza (FDL) na Daraja la Pili (SDL).

Mbali na Aishi, beki wa Yanga Juma Abdul amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa michuano hiyo huku mshambuliaji wa Ndanda, Atupele Green, akiwa Mfungaji Bora kwa mabao yake matano aliyopachika wavuni.

Vikosi vilikuwa hivi:

Azam FC: Aishi Manula, Erasto Nyoni, Gadiel Michael, Aggrey Morris, Abdallah Kheri, Jean Baptiste Mugiraneza, Himid Mao, Mudathir Yahya/Frank Domayo dk 63, John Bocco/Didier Kavumbagu dk 46, Ramadhan Singano ‘Messi’, Farid Mussa/Shaaban Idd dk 87.

Yanga SC: Deogratius Munishi, Juma Abdul, Oscar Fanuel/Mwinyi Mngwali dk 58, Kelvin Yondani, Vincent Bossou/Nadir Haroub ‘Cannavaro’ dk 87, Thabani Kamusoko, Simon Msuva, Haruna Niyonzima/Mbuyu Twite dk 65, Donald Ngoma, Amissi Tambwe, Deus Kaseke.

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.