Mshambuliaji huyo kutoka nchini Kenya aliyekuwa kwenye kiwango kizuri jana, aliiongoza Azam FC kupata ushindi wa mabao 2-1 katika mchezo huo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliofanyika Uwanja wa Mkwakwani Tanga huku bao la pili la matajiri hao likifungwa na beki Erasto Nyoni.
Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz mara baada ya mchezo huo Wanga alisema anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumsaidia kucheza vema na kudai kuwa atazidi kufanya vizuri kama akiendelea kupata nafasi katika mechi zilizobakia kabla ya msimu kumalizika.
“Kwanza namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kwa sababu naweza kusema sijakuwa na msimu mzuri vile nimezoea, nadhani kwa muda wangu wote niliocheza soka hapa Azam ndio sijacheza kwa kiwango changu, kufunga bao leo (jana), kusaidia Azam kushinda mechi hiyo naweza kusema ninafuraha na ni motisha kwangu,” alisema.
Wanga alisema kuwa anachoangalia kwa sasa ni kuendeleza kasi yake hiyo kuelekea mechi zijazo za mwisho za msimu ili kujiweka fiti, kurudisha hali ya kujiamini na kutoanza upya hata akiondoka kwenye kikosi hicho msimu ujao.
“Naweza kusema ni vizuri kwangu kupata ushindi leo (jana) na pia kucheza vile nilivyocheza, kwa sababu ni muda mrefu tangu nipate muda wa kucheza dakika 90,” alisema.
Mshambuliaji huyo aliendelea kusisitiza kuwa mambo yaliyochangia kumwangusha msimu huu tokea ajiunge na Azam FC ni kumpoteza Mama yake mzazi wakati msimu unaanza pamoja na kukosa maandalizi ya msimu mpya ya timu hiyo (pre season).
“Wakati narudi mechi zilikuwa zimeshaanza, nikakuta washambuliaji waliokuwa wanacheza walikuwa wanaonyesha kiwango kizuri, kwa hiyo sikupata ile nafasi haswa ya kuonyesha kiwango changu, ukiangalia tangu nimekuja Azam FC nadhani hii ndio mechi yangu ya pili naanza na nikacheza dakika 90.
“Kwa hiyo hali ya kukaa nje bila kucheza mechi nyingi, iliniathiri sana na ikafika mahali mimi kama mimi morali ikashuka kidogo, kwa sababu kila mchezaji sana sana unayeenda kucheza nje na wewe ni mshambuliaji, unakuwa na hali ya kutaka kucheza ili uweze kufunga na kuonyesha kiwango chako, jambo ambalo sikupata,” alimalizia Wanga.
Nyota huyo alijiunga na matajiri hao msimu huu akitokea El Merreikh ya Sudan alipogoma kuongeza mkataba mpya na kukimbilia nchini Afrika Kusini alipopata nafasi ya kufanya majaribio katika timu ya Bidvest Wits, ambapo alifanikiwa kufaulu lakini alishindwa kukamilisha taratibu za kujiunga na timu hiyo kutokana na kumuuguza Mama yake aliyekuwa katika hali mbaya ya kiafya kabla ya kutua Azam FC.
Mpaka sasa amefunga jumla ya mabao matatu msimu huu, mawili akifunga katika ligi dhidi ya Stand United na African Sports na jingine alitupia wakati Azam FC ikiitupa nje ya michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) timu ya Panone ya mjini Moshi kwa ushindi wa mabao 2-1.
0 Maoni:
Post a Comment