Wednesday, July 20, 2016

AZAM FC WAICHAPA FRIENDS GOLI 2-1

Posted By: dada - 5:20 PM

Share

& Comment

KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, imeendelea kujifua vilivyo kuelekea msimu ujao, ambapo katika kujiweka sawa leo Jumatno asubuhi imecheza mchezo wa kujipima ubavu dhidi ya Friends Rangers na kuifunga timu hiyo mabao 2-1.

Huo ni mchezo wa pili wa kirafiki wa maandalizi ya msimu mpya Azam FC ikiwa chini ya benchi jipya la ufundi kutoka nchini Hispania, linaloongozwa na Kocha Mkuu Zeben Hernandez, ambaye katika mechi ya kwanza aliifunga Ashanti United 2-0.

Kama kawaida katika mchezo huo, Zeben alikigawa katika makundi mawili kikosi chake, pia akiwajumuisha wachezaji watano waliokuwa kwenye majaribio ambao ni beki Mohamed Chicoto (Niger), mastraika Ibrahima Fofana (Ivory Coast), Bruce Kangwa (Zimbabwe), Mossi Moussa Issa (Niger) na Fuadi Ndayisenga (Burundi).

Kikosi cha kwanza kilichokuwa kikiundwa na kipa Aishi Manula, mabeki Gadiel Michael, David Mwantika, Aggrey Morris, Himid Mao, viungo Jean Mugiraneza, Khamis Mcha, Mudathir Yahya, washambuliaji  John Bocco, Shaaban Idd, Ibrahima Fofana kilicheza kipindi cha kwanza.

Kocha Zeben, aliingiza kikosi kingine kipindi cha pili akiwaingiza kipa Daniel Yeboah, mabeki Abdallah Kheri, Farid Mussa, aliyekuwa akicheza kama beki wa kushoto kabla ya kutolewa mwishoni na kuingia tena Gadiel, Ismail Gambo, Mohamed Chicoto, viungo Michael Bolou, Masoud Abdallah, Salum Abubakar na washambuliaji Bruce Kangwa, Mossi Moussa Issa, Fuadi Ndayisenga.

Vikosi vyote vilijitahidi kupambana kwenye mchezo huo na kupelekea kuambulia ushindi wa mabao 2-1, mabao ya Azam FC yakitupiwa na nahodha John Bocco na Mossi katika kila kipindi huku Cosmas Lewis akiifungia Friends Rangers inayofundishwa na Kocha wa zamani wa timu ya Vijana ya Azam, Kheri Mzozo.

Bocco alifunga bao la kwanza katika dakika ya 39 kwa shuti akimalizia mpira uliotemwa vibaya na kipa wa Friends kufuatia kupangua shuti lililochongwa na Mudathir Yahya, bao lililodumu hadi kumalizika kwa kipindi cha kwanza.

Lakini washambuliaji wa Yanga itabidi wajilaumu wenyewe kufuatia kupoteza nafasi takribani tano za kufunga mabao ndani ya kipindi hicho, hata katika kipindi cha pili mambo yalikuwa vivyo hiyvo.

Kasi ya wachezaji watatu waliokuwa kwenye majaribio, Moussa, Ndayisenga na Kangwa, ilizidi kuwachanganya Friends ambayo safu yao ya ulinzi ilikuwa ikikatika mara kwa mara na pia eneo la kiungo lililokuwa limeshikwa vilivyo na kinda wa Azam Academy, Masoud Abdallah ‘Cabaye’.

Haikushangaza kuona Azam FC ikiandika bao la pili dakika ya 77 kupitia kwa nyota aliokuwa kwenye majaribio, Mossi aliyemalizia vizuri kwa kuweka mpira wavuni kufuatia krosi safi ya Salum Abubakar ‘Sure Boy’.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki na NMB ingeweza kuongeza mabao zaidi kama mashuti mawili yaliyogonga mwamba yangejaa wavuni, moja likipigwa na Farid Mussa na jingine akipiga Kangwa kwenye dakika 20 za mwisho za mchezo huo.

Zeben afunguka vs Friends Rangers


Licha ya ushindi huo, Kocha Mkuu wa Azam FC, Zeben alipozungumza na mtandao wa rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz amesema kuwa hajafurahishwa na kiwango cha vijana wake kutokana na kutofanyia kazi baadhi ya mafundisho aliyowapa.

“Wachezaji hawajafanyia kazi mafundisho niliyowapa, mechi ya kwanza ilikuwa bora zaidi ukilinganisha na ya leo kwani ile ya kwanza wachezaji walijitahidi kufuata mafundisho niliyowapa, kilichobadilika leo walijitahidi kucheza na mipira,” alisema.

Alisema kuwa bado ataendelea kukipa mechi zaidi za kirafiki kikosi chake mpaka pale kitakapokuwa fiti huku akisisitiza kuwa hawezi kusema kwa sasa ni idadi ya mechi ngapi za kirafiki atakazocheza hadi kikosi chake kuwa kamili.

“Timu inaanza kuimarika na kucheza vizuri kwa sasa ukilinganisha na mwanzo, cha msingi hivi sasa ni wachezaji kushika mafundisho yote ninayowapa na kuyafanya kwa vitendo uwanjani,” alisema.

Baada ya mchezo huo, Azam FC kesho Alhamisi asubuhi itaendelea tena na mazoezi yake pamoja na Ijumaa kabla ya Jumamosi ijayo saa 3.30 asubuhi kucheza mchezo mwingine wa tatu wa kirafiki dhidi ya timu ya Halmashauri ya Kinondoni (KMC).

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.