Wednesday, August 10, 2016

USAJILI WA AZAM FC HUU HAPA, FARID KUELEKEA HISPANIA

Posted By: kj - 8:00 AM

Share

& Comment


UONGOZI wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, unayofuraha kubwa kuwatangazia kuwa imemaliza kikamilifu hatua ya kwanza ya usajili wa wachezaji kwa ajili ya msimu ujao.

Katika hatua hiyo ya kwanza iliyofungwa Jumamosi iliyopita saa 6.00 usiku, Azam FC tumewasajili jumla ya wachezaji 21 na kuwatoa wengine sita kwa mkopo.

Wachezaji wapya walioingia katika orodha hiyo ni mabeki Bruce Kangwa anayetokea Highlanders ya Zimbabwe, Daniel Amoah kutoka Medeama ya Ghana pamoja na winga Enock Atta Agyei (Medeama).

Mbali na nyota hao watatu wa kigeni, wachezaji wa msimu uliopita waliofanikiwa kupenya kwenye orodha hiyo ni makipa Aishi Manula, Mwadini Ally, mabeki Gadiel Michael, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Aggrey Morris, Pascal Wawa, David Mwantika na kinda Ismail Gambo ‘Kusi’.

Viungo ni Nahodha Msaidizi, Himid Mao ‘Ninja’, Jean Mugiraneza ‘Migi’, Michael Bolou, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Mudathir Yahya, Frank Domayo ‘Chumvi’, mawinga Ramadhan Singano ‘Messi’, Khamis Mcha ‘Vialli’ na mshambuliaji John Bocco ‘Adebayor’, ambaye ndiye Nahodha Mkuu wa kikosi.

Wanaotoka kwa mkopo  


Azam FC inayodhaminiwa na Benki na NMB na kinywaji safi kabisa cha Azam Cola, katika kukuza vipaji vya wachezaji wetu, tumeamua kuwatoa kwa mkopo nyota wetu wengine sita kwenda timu mbalimbali za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) na barani Ulaya.

Waliotolewa kwa mkopo hapa nchini, ni beki Abdallah Kheri tuliyempeleka Ndanda FC pamoja na kiungo Bryson Raphael, ambaye aliichezea timu hiyo msimu uliopita katika mzunguko wa pili na kuifungia mabao mawili.

Wengine ni winga Joseph Kimwaga aliyekwenda Mwadui baada ya kutakiwa na Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Jamhuri Kihwelu ‘Julio’, pamoja na washambuliaji Kelvin Friday aliyerejea Mtibwa Sugar na Ame Ally ‘Zungu’, aliyekwenda Simba.

Farid kutua Tenerife


Habari njema zaidi, tayari tumefikia makubaliano na Klabu ya Deportivo Tenerife ya Ligi Daraja la Pili Hispania (sawa na Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara), juu ya winga wetu wa kushoto Farid Mussa, waliyekuwa wakimuhitaji baada ya kufuzu majaribio ya kujiunga nao miezi mitatu iliyopita.

Hivyo, Farid hatakuwa sehemu ya kikosi chetu msimu ujao na anakwenda Tenerife ya huko, ambapo Azam FC kwa kutambua kipaji cha kijana wetu tumeamua tumwachie akajiunge na kikosi hicho kwa makubaliano maalumu na hatujachukua fedha yoyote kwa sasa lengo ni kuona kipaji chake kikikua zaidi na tunapenda kumtakia mafanikio mema huko anapokwenda.

Tunaamini mafanikio yake yoyote huko, atakuwa amelitangaza vema jina la Azam FC na kadiri atakavyokuwa akizidi kusonga mbele basi hapo ndipo klabu yetu itakuwa ikinufaika zaidi kupitia biashara hiyo.

Usajili hatua ya pili


Katika kumalizia taratibu zote za usajili kwa msimu ujao, Azam FC bado tunaendelea na zoezi hilo la usajili kwa hatua ya pili likihusisha wachezaji wa kigeni, ambalo litaanza rasmi Agosti 17 hadi Septemba 7, mwaka huu.


IMETOLEWA NA UONGOZI WA AZAM FC,
AGOSTI 9, 2016.

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.