Thursday, August 18, 2016

ZEBEN AZUNGUMZIA MCHEZO NA YANGA, AZAM KUFUNGUA VPL USIKU

Posted By: kj - 8:06 PM

Share

& Comment

SAA chache mara baada ya kikosi chake kushinda taji la Ngao ya Jamii, Kocha Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Zeben Hernandez, amesema kuwa timu yake inauwezo wa kufanya vizuri zaidi msimu huu kama wachezaji wake watashika kile anachowafundisha.

Azam FC jana jioni iliweza kuandika historia mpya ya kulitwaa kombe hilo baada ya kulikosa mara tatu mfululizo ikiifunga Yanga kwa mikwaju ya penalti 4-1 kufuatia sare ya mabao 2-2 ndani ya dakika 90.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Zeben alisema kuwa cha muhimu kwake hivi sasa ni kufanya kazi vizuri na kuwapa elimu wachezaji wake ili kupata mafanikio na kuwa timu bora msimu huu.

“Wachezaji kama kweli wakishika kile ninachowaelekeza uwezekano mkubwa wa kushinda utakuwepo, siwezi kusema tutashinda mataji yote kwani huu ni mpira chochote kinaweza kutokea, lakini naamini uwezo wa kufika mbali zaidi upo cha muhimu ni wachezaji kushika mafundisho ninayowapa,” alisema.

Auzungumzia mchezo vs Yanga

Akizungumzia mchezo huo, Zeben alisema kuwa ana furaha kubwa mara baada ya kutwaa ubingwa huo huku akikiri kuwa timu yake ilishindwa kuonyesha kiwango kizuri katika kipindi cha kwanza.

“Ninafuraha kubwa ukizingatia kipindi cha kwanza hakikuwa kizuri, lakini mara baada ya kufanya mabadiliko ya wachezaji kipindi cha pili ikazaa matunda ya ushindi huo, wachezaji niliowaingiza waliweza kufanya kile nilichowaahidi hadi tukaweza kurejea mchezoni na kushinda, kiukweli nakifurahia sana kikosi changu,” alisema.

Kocha huyo wa zamani wa Santa Ursula alisema aliweza kukisoma kipindi cha kwanza na kuweza kufanya mabadiliko ya mfumo na uchezaji jambo ambalo liliwapa matokeo.

“Nilikisoma kipindi cha kwanza na baadaye nikaona cha msingi ni kwamba ni kubadilisha mchezo na nilijaribu kuwapa maelekezo wachezaji kuongeza umakini, tuliweza kuwazawadia mpira Yanga na baadaye wakajikuta kuwanatupa mipira hiyo na wao kutoka nje ya mchezo hali iliyotufanya sisi kurejea na kushinda,” alisema.  

Moja ya mambo makubwa yaliyoiongezea kasi Azam FC kipindi cha pili ni kocha Zeben kuongeza kasi ya mashambulizi pembeni ya uwanjani kwa kumpeleka kulia Shomari Kapombe aliyekuwa akicheza eneo la ulinzi wa kati na kumpa uhuru Bruce Kangwa wa kupanda upande wa kushoto kusaidia mshambulizi.

Mbali na hilo pia alimrejesha katikati kipindi cha pili kiungo Salum Abubakar, aliyekuwa akipeleka mashambulizi kutokea kulia (namba saba) kipindi cha kwanza, ambaye aliweza kuimarisha eneo la kiungo akishirikiana vema na Mudathir Yahya aliyeingia kipindi cha pili.

Pia kuingia kwa straika mpya, Francisco Zekumbawira, kuliweza kuliimarisha eneo la ushambuliaji la Azam FC baada ya mshambuliaji huyo kushirikiana vema na nahodha John Bocco, ambao wote waliweza kuilinda mipira yote iliyokuwa ikiletwa eneo hilo.

Hali hiyo iliweza kuleta madhara makubwa kwenye lango la Yanga na hatimaye ikarejesha mabao yote mawili kupitia kwa Shomari Kapombe na lile la mkwaju wa penalti lililofungwa na Bocco na kama Kangwa angekuwa na umakini dakika za mwisho za mchezo huo basi isingeshuhudiwa hatua ya matuta.

Kangwa alikuwa katika nafasi nzuri ya kuandika bao la pili kwa Azam FC kabla ya penalti iliyozaa bao la kusawazisha, lakini kichwa alichopiga akiwa ndani ya eneo la 18 kiliweza kugonga chini na kugonga mwamba wa juu kabla ya mpira kuokolewa na mabeki wa Yanga.

Safari ya VPL yaanza 


Wakati Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB na kinywaji safi cha Azam Cola ikianza kwa vema msimu huu kwa kutwaa taji hilo kama ilivyofanya msimu uliopita kwa kubeba Kombe la Kagame, inatarajia kuanza safari yake ya kufukuzia ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzani Bara (VPL) keshokutwa Jumamosi kwa kumenyana na African Lyon.

Mchezo huo unaotarajia kuwa mkali na wa aina yake utafanyika kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, ambapo awali ulitakiwa upigwe saa 10.00 jioni, lakini Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limebadili muda na kuupeleka hadi saa 1.00 usiku.

TFF imebadilisha muda huo, ili kuiwezesha timu ya Taifa ya vijana ya Afrika Kusini (U-17) ‘Amajimbos’ kuweza kuutumia uwanja huo saa 9. 00 Alasiri siku hiyo kufanya mazoezi yake kama sheria za Shirkisho la Soka Afrika (CAF) zinavyotaka kabla ya kurudiana na vijana wa Tanzania ‘Serengeti Boys Jumapili ijayo.

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.