Sunday, March 4, 2018

AZAM FC WAIFUMUA SINGIDA UNITED

Posted By: dada - 7:46 AM

Share

& Comment

KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imezidi kufanya kweli baada ya kuichapa Singida United bao 1-0 kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliomalizika Uwanja wa Azam Complex usiku huu.

Matokeo hayo yanaifanya Azam FC kuzidi kujiweka vizuri kwenye msimamo wa ligi hiyo na pia kuongeza pengo la pointi  baina yake ya Singida United na kufikia nne ikifikisha pointi 38 katika nafasi ya tatu huku Simba ikiwa kileleni kwa pointi 46 na Yanga yenye mchezo mmoja mkononi ikiwa nazo 40 (nafasi ya pili).

Azam FC ilianza kwa kasi kwenye mchezo huo hali iliyopelekea kupata bao la mapema dakika ya 16 lililofungwa na winga Joseph Mahundi, aliyepiga shuti zuri lililomshinda kipa wa Singida, Ally Mustapha ‘Barthez’, akiitumia vema pasi ya Mbaraka Yusuph.

Bao hilo liliweza kudumu hadi mwisho wa mchezo huo, ambapo ilishuhudiwa kipa wa Azam FC, Mwadini Ally, akiibuka nyota wa mchezo baada ya kuokoa michomo hatari ya wachezaji wa Singida huku pia mshambuliaji Yahya Zayd na Mbaraka Yusuph wakionyesha kiwango bora wakiwasumbua muda mwingi wa mchezo mabeki wa timu pinzani.

Safu ya ulinzi ya Azam FC iliyokuwa ikiundwa na nahodha msaidizi, Agrey Moris, Abdallah Kheri, Bruce Kangwa na David Mwantika, nayo ilifanya kazi kubwa ya kuzuia mashambulizi ya Singida United, hasa kipindi cha pili baada ya wapinzani hao kuja juu wakitafuta bao la kusawazisha.

Mwadini aliyekuwa kwenye kiwango bora akiondoka uwanjani bila nyavu zake kutikiswa, alirejea langoni leo baada ya kipa namba moja Razak Abalora, kusimamishwa na Bodi ya Ligi.

Mara baada ya mchezo wa leo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kupumzika kesho Jumapili kabla ya kuanza maandalizi Jumatatu jioni ya kujiandaa na mchezo ujao dhidi ya Mwadui utakaofanyika Alhamisi ijayo na ule wa Mbao Jumapili ijayo, yote ikifanyika Uwanja wa Azam Complex saa 1.00 usiku.

Kikosi cha Azam FC leo:
Razak Abalora, David Mwantika, Abdallah Kheri, Agrey Moris (C), Stephan Kingue, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Frank Domayo, Yahya Zayd/Salmin Hoza dk 90+4, Mbaraka Yusuph/Shaaban Idd dk 65, Joseph Mahundi/Enock Atta dk 28

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.