KOCHA wa Azam, Stewart Hall ameanika mikakati yake ya msimu ujao na kuzionya Simba na Yanga kuwa anataka ubingwa wa Tanzania Bara.
Hall, ambaye amewahi kuwa Mkurugenzi wa Soka wa Birmingham inayoshiriki Ligi Kuu England, aliiambia Mwanaspoti anataka kuudhibiti umwamba wa timu hizo kongwe kwenye Ligi Kuu.
Akizungumza na Mwanaposti jana Ijumaa kwenye mazoezi ya timu yao kwenye Uwanja wa Mbande-Chamazi unaomilikiwa na klabu hiyo nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, alisema wamefanya usajili makini unaomfanya ajiamini msimu ujao.
Nyota wa kigeni waliosajiliwa katika kikosi hicho ni Kipre Tchetche (Ivory Coast), Obren Cirkovic (Serbia) na raia wa Ghana, Abdul Wahab Yahya na Nafiu Awudu wanaoungana na Mkenya Ibrahim Shikanda wa Kenya.
Wachezaji wapya wa Kitanzania waliosajiliwa msimu huu ni Said Morad, Abdulhalim Humoud, Zahoro Pazi, Mwadini Ally, Ghulam Ally na Mohamed Selembe.
Hall alidai wameandaa mikakati kambambe ya kuifanya Azam itambe si Tanzania tu bali Afrika nzima. "Tunataka ubingwa au nafasi ya pili halafu kitakachofuata ni kufanya vyema kwenye mashindano ya Afrika," alisema Hall, ambaye ana kawaida ya kuwapa wachezaji wake ndizi na mayai baada ya mazoezi.
Hall alieleza kwamba ameanza kuwajenga stamina kwa kuwapeleka gym wachezaji wake ili wawe fiti kwa mazoezi ya uwanjani.
Wachezaji 18 walifanya mazoezi jana Ijumaa wakiwemo wapya Kipre, Morad, Humoud, Pazi, Mwadini, Ghulam na Selembe. Nyota wa Ghana wanatarajiwa kuwasili nchini Juni 23 ili kuungana na wenzao wakati Obren atafika kesho Jumapili na ataanza mazoezi keshokutwa Jumatatu.
source: mwanaspoti.co.tz
Sunday, June 19, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Maoni:
Post a Comment