Saturday, June 25, 2011

Mazoezi yapamba moto

Posted By: kj - 8:37 PM

Share

& Comment

Mazoezi ya maandalizi ya msimu wa ligi kuu ya Vodacom 2011/12 yameanza kwa matumaini makubwa sana kwenye kikosi cha Azam FC ambacho kimesukwa upya na kocha mkuu Stewart Hall akisaidiana na msaidizi wake Kally Ongala.

Ni wiki mbili tangia mazoezi yaanze sasa, cha kufurahisha ni kwamba wachezaji wote wa Azam FC wamekuwa wakifika mazoezini bila kukosa kwa siku zote hizo 12 isipokuwa Zahoro Pazi pekee ambaye alikosa mazoezi kwa siku mbili kutokana na kuugua tumbo.

Wachezaji wa Azam FC wamekuwa na programu kabambe ya mazoezi ambapo wamekuwa wakifanya mazoezi Gym kwa siku za Jumatatu, Jumatano na Ijumaa huku wakichezea mpira siku za jumanne, Alhamisi na Jumamosi.

Stewart Hall, kocha toka uingereza mwenye uweledi mkubwa sana wa soka anasema programu kama hii ndiyo muafaka na ndiyo ambayo imekuwa ikitumiwa na vilabu vikubwa duniani wakati wakipindi cha maandalizi. Kuna mambo mengi yakufurahisha kwenye mazoezi ya Azam FC lakini kubwa zaidi ambalo halijawahi kuwepo huko nyuma ni ushindani uliopo katika kugombania namba.

Wachezaji wamekuwa wakijituma sana mazoezini na kila mchezaji anatambua kwamba haitakuwa rahisi kwake kupata namba kwenye kikosi cha kwanza hivyo wanapaswa kufanya kazi kwa bidii.

Sehemu ya kiungo ndiyo ambayo imekuwa gumzo zaidi msimu huu, mchezaji Ibrahim Rajab Jeba licha ya kuwa na umri wa miaka 16 pekee amekuwa aking’ara sana mazoezini na kuwapa changamoto wachezaji wazoefu. Eneo hili la kiungo limemshuhudia mchezaji Abdulghani Ghulam Abdallah akifunika katika mechi zote zama zoezi. Abdulhalim Humud, Ramadhani Chombo Redondo na Ibrahim Mwaipopo wamekuwa wakicheza kandanda safi sana na kuwafanya watu kujiuliza hali itakavyokuwa pindi Jabir Aziz, Himid Mao na Salum Abubakar watakaporejea kikosini toka kwenye kikosi cha U-23.

Katika mazoezi ya leo, Kipre Herman Tchetche alifunga goli moja kwa timu yake na kufanya matokeo yawe 1-0 kwa timu ya wachezaji wapya wakiwafunga wachezaji wa zamani. Goli laTchetche lilikuwa la tano mazoezini tangia ajiunge na Azam FC akiwa ni mchezaji pekee aliyefunga kila mechi mazoezini, wachezaji wengine waliokwishafunga ni Ngasa goli 1, Ghulam goli 1, Luckson goli 1, Mwaipopo goli 1, Rooney goli 1 na Bocco goli 1.

Ni dhahiri mwalimu Stewart Hall atakuwa na kazi kubwa ya kuamua nani aanze golini kati ya Mwadini Ally ambaye yupo katika kiwango cha hali ya juu sana na Mserbia Obren Cuckovic. Upande wa beki wa kushoto, Ibrahim Shakanda anapewa changamoto kubwa na Erasto Nyoni ambaye katika mchezo wa leo alikuwa nyota wa mchezo.

Upande wa beki wa kushoto kwa sasa Waziri Salum Omar anaonekana kuidhibiti nafasi hiyo lakini Samih Haji Nuhu ambaye ni majeruhi anaendelea kupona kwa haraka hivyo endapo Haji atakuwa amepona na ubora wa kiwango cha Malika Philip Ndeule kutamfanya Waziri kuongeza juhudi kama atapenda kukabidhiwa jukumu la kusimama upande wa kushoto.

Beki wa katikati ndiyo balaa, Azam FC imesajili mabeki wawili wa katikati, Nafiu Awudu ambaye ni nahodha wa timu ya taifa ya Ghana Black Stars inayohusisha wachezaji wa ndani na Said Morrad toka kagera Sugar ambao wanaungana na Aggrey Morris na Luckson Kakolaki. Ubora wa mabeki wote hawa unafanya sehemu hii kuwa ngumu kutabiri nani ataanza. Itakuwa kazi kwa kocha kuamua nani aanze lakini itakuwa kazi kubwa zaidi kwa wachezaji wenyewe kumshawishi mwalimu kutokana na upinzani mkali uliopo.

Azam FC ina mawinga watano ambao ni Selemani Kassim Selembe, Jamal Mnyate, Khamis Mcha Viali, Mrisho Ngasa ambaye ni mfungaji bora wa Vodacom Premier League na Kipre Tchetche ambaye ni mchezaji bora wa ligi kuu ya Ivory Coast. Baada ya kutaja wachezaji hao mtandao wa azamfc.co.tz unakuachia msomaji jukumu la kutabiri nani ataanza na nani atakaa benchi.

Azam FC imesajili washambuliaji watatu ambao ni Zahoro Pazi, John Bocco na Wahab Yahaya. Hadi sasa wachezaji hawa wanaonekana kuwa na sifa tofauti, wakati Bocco akiwa nasifa ya urefu, uwezo wa kupiga vichwa na uwezo wa kujipanga. Wahab anaonekana kuwa nakasi, Nguvu, na uwezo mkubwa wa kumiliki mpira huku Zohoro akiwa na kipaji cha kipekee cha kuuchezea mpira, spidi na ujanja. Mtandao wa azamfc.co.tz hauwezi kutabili nani ataanza nanani atasubiri benchi.

Azam FC imepanga kuanza mechi za majaribio wiki tatu kuanzia leo yaani tarehe 15 July.


chanzo: www.azamfc.co.tz

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.