UKITAJA wachezaji zao la michuano ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 ‘Copa Coca Cola’, hutosika kumjumuhisha kutokana na umahiri wake sasa. Huyo ni Himid Mao Mkami, kiungo wa timu ya Azam FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara . Haya ni mahojiano kati ya shaffih dauda sport blog na Himid.
Unaweza kutueleza ulizaliwa mwaka gani na wapi?
Nimezaliwa Novemba 5 , mwaka 1992 , Kinondoni jijini Dar es Salaam, baba yangu ni Mao Mkami, mchezaji wa zamani wa Pamba ya Mwanza.
Unaweza kututajia timu unayoishabikia tangu utotoni?
Mimi ni shabiki mkubwa wa Chelsea ya England, lakini pia naihusudu klabu ya mtaani kwangu ya Kagera Rangers.
Ipi silaha yako kubwa uwapo uwanjani?
Silaha yangu kubwa niwapo uwanjani ni uwezo wangu wa kukaba adui na kuwa katika nafasi yangu kila wakati.
Nini upungufu wako uwapo uwanjani?
Sipendi kukaba nikiwa mchezoni, japokuwa ni kitu ambacho ni silaha yangu; wakati mwingine nashindwa kumzuia mtu ambaye baadaye analeta madhara.”
Ni mchezaji yupi unaweza kumtaja kama shujaa kwako?
Marcos Senna (kiungo mkabaji wa Villarreal CF ya Hispania), ndiye shujaa wangu katika soka, napenda kucheza soka kama anavyocheza yeye .
Unahisi unacheza kama mchezaji yupi uwapo uwanjani?
Binafsi najiona nacheza kama Kaka’ wa Real Madrid.:
Nini matarajio yako katika soka?
Nawaza kucheza soka la kulipwa siku moja, tena katika klabu kubwa kama Real Madrid ya Hispania, nitawashawishi mawakala kwa kujituma zaidi kila siku :
Ni siku ipi ulihuzunika zaidi katika maisha ya soka?
Hakuna siku niliyohuzunika katika maisha yangu ya soka kama siku tulipofungwa na Nigeria katika mchezo wa nusu fainali ya vijana kwenye michuano ya International Coca Cola. Nilikuwa Nahodha wa Timu ya Taifa ya Vijana wenye umri chini ya miaka 17 , ‘Serengeti Boys’, tulifungwa mabao 2-1 japokuwa awali tulijiamini kushinda mechi hiyo.
Unaweza kumtaja nani kuwa ni mchezaji bora unayemuona hadi sasa?
Ni Salum Aboubakar Salum ‘Sure Boy’, ndiye mchezaji bora kwangu hadi sasa, huyu anatoa pasi safi na nzuri wakati wote uwanjani.
Mchezaji yupi unamuona mtukutu, lakini ni kiburudisho katika timu?
Napenda sana kufurahi kila mara; naweza kumtaja Salum Machaku wa Simba kuwa ndiye mchezaji pekee nchini anayenichekesha kila mara, huyu hupenda utani kila wakati, alikua anatupunguzia msongo wa mawazo tuwapo kambini au mazoezini pindi alipokua anachezea Azam.
Unapenda aina ipi ya muziki?
Napenda sana muziki wa hip hop, navutiwa na Kanye West hasa kupitia wimbo wake wa ‘You can’t tell me nothing’. Lord Eyes ni mwana hip hop wa Tanzania anayenivutia.
Aina ipi ya gari unayoipenda?
Napenda sana magari aina ya BMW, linaweza kuwa gari la kwanza kulinunua endapo nitajaliwa kupata fedha za kuweza kufanya hivyo.
Filamu ipi unayoipenda, na kwa sababu gani?
Apocalypto ndiyo filamu niipendayo (iliyotoka mwaka 2006 iliyoongozwa na Mel Gibson, ikiwa imeigizwa huko Amerika ya Kati katika jamii ya Maya), katika filamu hiyo kuna matukio mengi ya kijasiri (ikiwemo safari ya kabila la Mesoamerican lililotekwa), lakini muigizaji (mkuu Jaguar Paw (Rudy Youngblood), amenivutia zaidi kutokana na uhodari wake.
Je, unaweza kutueleza jambo lolote tusilolijua kuhusu wewe?
Kweli, sipendi kuonekana kama staa kama wafanyavyo mastaa wengine wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Mimi ni mtu wa kawaida sana, nafurahi zaidi kujiona nipo sawa na watu wengine katika jamii kila wakati.
Ni kipi ambacho ungekifanya endapo usingekuwa mwanasoka?
Moja kwa moja ningekuwa mwanamuziki, tena wa hip hop. Ningependa kuimba nyimbo za kuiasa jamii kuhusu ugonjwa wa UKIMWI.
Unaweza kuueleza ni ushauri upi unaouona kuwa bora uliopewa katika soka?
Kaka Shaaban Kisiga niliyecheza naye Azam aliwahi kunipa ushauri mzuri sana ambao nautumia hadi leo, huyu aliwahi kuniambia; “Kila wakati heshimu maamuzi yako”.
Ulinunua kitu gani ulipopata fedha yako ya kwanza katika soka?
Nakumbuka fedha yangu ya kwanza kupata nikiwa katika soka ni ile ya posho ya Serengeti Boys mwaka 2007 , nililipwa Sh 180 ,000. Nilinunua simu aina ya Siemens yenye kamera, kwa bahati mbaya iliharibika ndani ya wiki moja tu, nilihuzunika sana.
Ni mwanadada yupi unayemuhusudu?
Nampenda sana mwanamuziki wa R&B, Keri Lynn Hilson wa Georgia, Marekani kuwa ni mwanadada ninayemhusudu kupita wote, na kama ningepata nafasi ya kukutana naye ningefurahi kupita kiasi. Navutiwa na wimbo wake uitwao Knock You Down.
copied from shaffih dauda sports blog
Tuesday, July 12, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Maoni:
Post a Comment