NYOTA njema imemwakia mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania wa klabu ya Azam FC, Mrisho Ngassa baada ya kuanza vizuri harakati zake za kusaka nafasi ya kucheza soka ya kulipwa katika timu ya Seattle Sounders ya Marekani. Ngassa aliondoka nchini Julai 9 na aling’ara katika mazoezi ya timu hiyo na hivyo kupewa nafasi kubwa ya kuanza katika mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Manchester United hapo Julai 20.
Akizungumza kwa njia ya simu, Rahim Kangezi aliyefanikisha ziara ya Ngassa nchini Marekani alisema mchezaji huyo hivi sasa anafanya mazoezi katika timu ya kwanza na anazidi kufanya vyema. Kangezi alisema majaribio hayo yamempa faraja kubwa Ngassa tangu alivyojiunga na timu hiyo na upo uwezekano mkubwa wa kuanza katika mechi dhidi ya Manchester United kama kiungo wa pembeni (winga).
“Nimefurahi kuambiwa Ngassa amevutia sana benchi la ufundi la timu ya Seattle Sounders, wamefurahia kiwango chake, naamini atafanya vizuri na kuipa Tanzania historia mpya katika medani ya soka,” alisema Kangezi. Kangezi alisema Ngassa ameonyesha kujituma zaidi katika majaribio hayo na bila shaka hatarejea kucheza ligi ya Tanzania tena.
Alisema kuwa ‘ndoto’ ya mchezaji huyo ni kucheza soka la kulipwa baada ya kushindwa nchini Uingereza katika timu ya West Ham miaka ya nyuma. Alisema kuwa kama atafanikiwa, atakuwa mtanzania wa pili kucheza ligi ya Marekani, baada ya Nizar Khalfan anayechezea timu ya Vancouver Whitecaps ya Canada.
Kiasi gani cha fedha timu hiyo itatoa baada ya Ngassa kufaulu kitafahamika baadaye.
Copied from mwananchi.co.tz
Wednesday, July 13, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Maoni:
Post a Comment