MSHAMBULIAJI wa Azam FC, Mrisho Khalfan Ngassa amesema kitendo cha kuivaa Manchester United ya Ligi Kuu wakati wa majaribio yake ya Marekani kimefungua njia ya kutimiza ndoto yake ya kucheza soka nje ya Tanzania.
Ngassa anasema licha ya kucheza dakika chache, bado ilisaidia makocha wa timu ya Seattle Sounders alikokuwa anajaribiwa kupima uwezo wake licha ya timu yao kuchakazwa na Manchester United 7-0 kwenye mechi ya kujipima nguvu kati ya timu hizo mbili.
Ngassa sio siri ni mwanasoka nyota wa Tanzania kwa sasa kutokana na mchango wake mkubwa Taifa Stars na kwenye timu yake ya Azam. Wadau wa soka siku nyingi wame kuwa wa kijiuliza inakuwaje Ngassa anang'ang'ania kucheza Tanzania pamoja na kujaliwa kasi na umahiri katika kufunga.
Sasa kitendo cha kujaribiwa na Seattle Sounders na kucheza dhidi ya mabingwa wa soka wa England, Manchester United ni wazi sasa kina wapa matumaini Watanzania kuwa hazina yao sasa itapata timu na kung'arisha kipaji chake nje ya mipaka yaTanzania.
Ngassa aliwahi kufanya majaribio katika timu ya WestHam ambako hakusajiliwa na pia alitakiwa kusajiliwa na Lov-Ham ya Norway. Kuna wakati alipata pia timu Russia. Hata hivyo, majuzi Ngassa alikwenda Marekani kwa majaribio ya wiki tatu katika klabu ya Seattle Sounders.
Akiwa na klabu hiyo Ngassa aliandika historia ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Manchester United. Ngassa aliingizwa katika dakika15 za mwisho za mchezo huo. Akiwa huko Ngassa amelielezea Mwanaspoti mambo mbalimbali aliyokutana nayo katika kipindi chote cha majaribio na jinsi anavyo ifikiria hatma yake.
MAJARIBIO YAKE
Ngassa ameeleza majaribio yake na kusema; "Haikuwa jambo rahisi au gumu kwa sababu siku zote mpira hauna tofauti isipokuwa ni uwajibikaji na ufundi, unajua hata kwenye chakula tofauti iko katika mapishi. "Kulingana na majaribio yangu naamini mambo yameenda vizuri kwa sababu majaribio, nimefanya vizuri katika kiwango walichokitaka na naamini uwezo wangu utanirudisha tena kwa mara nyingine, nafikiri walioniona wameshuhudia uwezo wangu wakati wa mechi na Manchester United," anasema Ngassa, mtoto wa kiungo wa zamani wa Pamba, Simba na Taifa Stars, Khalfan Ngassa.
Ngassa anasema alipofika makocha wa Sounders walikuwa wanamwona kama hajui; "Unajua nilipofika awali walikuwa hawaniamini kabisa wakiniona kama sijui vile. "Si unajua sehemu yoyote unapofika mgeni, wana kuwa na wasiwasi na wewe, lakini kwasababu najiamini nikasema nataka kufanya kazi nikawa makini kusubiri siku ya mechi na Manchester United ili kuonyesha uwezo wangu," anasema Ngassa ambaye ana mhusudu Lionel Messi na anatamani siku moja afikie alipo.
TOFAUTI NA CHANGAMOTO
"Asikwambie mtu ni kwamba wenzetu wako mbele kwa kila kitu na hata katika utendaji ni hivyo hivyo tofauti nasisi," anasema Ngassa, ambaye ni baba wa watoto wawili, Farida na Junior.
Ngassa anaeleza kuwa tofauti kubwa aliyokutana nayo ni katika mazoezi; "Kusema kweli tofauti na changamoto niliyo kutana nayo kwa wenzetu wako makini. "Wao wanajali mazoezi kuliko kitu kingine chochote na ndiyo tofauti kubwa yao na sisi, kule hakuna utani hata kidogo, muda wa mazoezi una heshimiwa. "Ukifika muda wa mazoezi unatakiwa kufika kwa wakati, lakini pia unapo kuwa katika mazoezi hakuna utani."
Ngassa anaeleza alicho kikuta katika benchi la ufundi; "Benchi la ufundi la ile timu wako makocha wanne na kila mmoja ana kazi yake, yupo wa viungo, makipa, kocha msaidizi anayesimamia mazoezi. Kocha Mkuu hasimamii mazoezi hivyo labda kama ana kitu maalumu anataka kuelekeza.
MECHI YA MANCHESTER
Akizungumzia mechi ya Manchester United, Ngassa anasema kuwa; "Haikuniogopesha sana licha ya kuwa kwangu imenijenga, kama unavyojua Manchester United ni timu kubwa kwa hiyo kwangu ni faida kukutana nayo. "Hata hivyo, sikuwa na woga kwani nikiwa Taifa Stars nilishawahi kucheza mechi na timu ngumu za Brazil, Ivory Coast na Cameroon na wachezaji wao ni mastaa kwenye soka ndiyo maana nilichukulia kama mchezo wa kawaida tu na sio kwamba nilibabaika. Anaeleza kuwa, katika mchezo huo aliweza kuwamudu vyema wapinzani wao kutokana na uzoefu wa mechi mbili. "Nilikabiliana vizuri na mabeki wa Manchester United na hasa Fabio, kwa kweli siku waogopa kwani kisaikolojia nilichukulia sawa na mechi nyingine."
MAGENI ALIYOKUTANA NAYO
"Yapo mageni, lakini siyo mapya labda vitendea kazi wenzetu wako juu, wame endelea na hilo la kuzingatia mazoezi kama nilivyo kuambia."
MAZINGIRA NA MATAZAMO WAKE
Ngassa anasema; "Mazingira ni mazuri sana, kama nilivyosema wenzetu wametuzidi kiujumla, yanafaa sana kwa maisha ya mpira na yana mfanya mchezaji kupenda kazi yake zaidi na zaidi. "Kwa upande wa majaribio nimefanya vizuri kama mlivyo ona wenyewe kwenye mechi na Manchester United."
MRISHO KHALFAN NGASSA
Amezaliwa: Mei 5, 1989,
Mahali: Mwanza
Klabu alizochezea: Toto African 2004-2006, Kagera Sugar 2006-2007, Yanga 2007-2010, Azam FC 2010
Timu za Taifa: Taifa Stars, Kilimanjaro Star, Ngorongoro Heroes.
Chanzo: mwanaspoti.co.tz
Tuesday, August 2, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Maoni:
Post a Comment