Tuesday, October 18, 2011

Ngassa kama Van Persie

Posted By: kj - 10:45 AM

Share

& Comment

MSHAMBULIAJI wa Azam FC, Mrisho Ngassa, amefuata nyayo za mshambuliaji wa Arsenal, Robin van Persie, kwa kufunga bao la mapema zaidi kwenye mechi ya soka.

Ngassa ambaye alilifukuzia mbali jinamizi la ukame wa mabao kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kufunga kwenye mechi na JKT Ruvu, Jumamosi iliyopita, alifunga katika sekunde ya 36. Azam ilishinda mabao 2-0.

Bao hilo lilifananishwa na lile la Mholanzi Van Persie ambaye alifunga sekunde ya 27 wakati Arsenal ilipoiliza Sunderland mabao 2-1 katika Ligi Kuu England Jumapili.

Van Persie naye kama Ngassa, bado hajawaweza kuvunja rekodi za kufunga mabao ya mapema zaidi kwenye ligi zao.

Ngassa kwa mfano hajaweza kuvunja rekodi ya mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Boniface Ambani, ambaye alifunga katika sekunde ya 20 dhidi ya Coastal Union ya Tanga katika msimu wa 2008/09.

Pia Van Persie hajavunja rekodi ya beki wa Tottenham Hotspur, Ledley King, aliyefunga katika sekundi ya 10 dhidi ya Bradford mwaka 2000.

Ngassa aliyekuwa mfungaji bora msimu uliopita kwa kupachika mabao 16, angalau amepata bao la kwanza kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu.

Winga huyo anayeichezea pia timu ya taifa, Taifa Stars, alifunga baada ya kuwazidi ujanja mabeki, Damas Makwaya na Shaibu Nayopa, kabla ya kumtungua kirahisi kipa Shabaan Dihile. John Boko ndiye aliyefunga bao la pili dhidi ya JKT.

Ngassa sasa ameungana na washambuliaji KipreTchetche (Azam FC), Gervais Kago (Simba) na Mohamed Kijuso (Villa Squad) waliofunga mabao ya mapema msimu huu.
Naye kocha wa Azam, Stewart Hall, alisema baada ya pambano hilo kuwa amefurahi kumwona Ngassa akirejea katika makali yake ya ufungaji.

mwanaspoti.co.tz

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.