Tuesday, November 1, 2011

Moradi: Angoja wakati wake wakuitwa stars

Posted By: kj - 6:17 PM

Share

& Comment


HAKUNA ubishi kuwa beki, Said Morad, ndiye nguzo ya safu nzima ya ulinzi ya Azam FC, ambayo imefungwa mabao machache zaidi kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara inayoendelea nchini.

Morad akishirikiana na Aggrey Morris na mabeki wa pembeni, Wazir Omary upande wa kushoto na Erasto Nyoni anayecheza kulia, wameifanya timu hiyo kuwa na ukuta mgumu zaidi.

Beki huyo mwenye mkataba wa mwaka mmoja utakaofika tamati mwishoni mwa ligi, uimara wake, ushupavu, sifa ya kutoremba mpira na matumizi ya akili, vimemfanya kuwa kikwazo kwa washambuliaji wa timu nyingine za ligi hiyo.

Simba na Yanga ndiyo zinaaminika kuwa timu zenye washambuliaji hatari zaidi, lakini zote hazikutikisa nyavu za Azam zilipokutana nayo. Azam iliifunga Yanga bao 1-0 na kutoa suluhu na Simba ikiwa matunda ya mabeki wa timu hiyo.

Morad ni mrefu na mwembamba kwa umbo, jambo linalompa uhuru wa kufanya lolote analolitaka akiwa dimbani. Kwa uhodari wake, amefanikiwa kumweka benchi, Nafiu Awudu, kutoka Ghana, ambaye aliigharimu Azam fedha nyingi.

Mwanaspoti ilimtafuta Morad kwa ajili ya kumfahamu zaidi maisha yake, mafanikio na malengo aliyonayo katika soka.

Morad anaishi Ilala, jijini Dar es Salaam katika Mtaa wa Songea karibu na msikiti wa Songea, nyuma ya jengo la Machinga Complex. Ni karibu na maskani ya timu ya Young Stars, ambayo kwa kiasi kikubwa ilichangia kuonekana kwa soka lake kabla ya kutua Ligi Kuu.

Kilichomngarisha Azam

Azam si timu yake ya kwanza Ligi Kuu. Morad alishachezea timu za Ashanti na Kagera Sugar.

"Kungaa kwangu kunatokana na kuwa na kipaji na ndiyo ikachangia kusajiliwa na Azam", anasema Morad anayehusudu soka la Nemanja Vidic wa Manchester United, klabu ambayo pia anaishabikia kwa Ulaya.

"Unajua ukiwa mikoani hata kama una kipaji namna gani, si rahisi kuonekana tofauti na ukiwa unacheza timu za hapa jijini hasa zenye majina kama Simba, Yanga na sasa Azam."

"Lakini mikoani kuna vipaji kuliko hata vya wachezaji wenye majina makubwa Simba na Yanga, tatizo hawapati nafasi za kuonekana. Timu kama Kagera Sugar, JKT Oljoro au Polisi Tanzania, kuonekana kwake mpaka zikija kucheza Dar es Salaam na Simba na Yanga."

"Mambo yote ya maendeleo ya soka yapo mjini, huko porini hakuna kitu, mpaka ubahatike, mtu aje kukuchukua, ndiyo unajulikana."

Kutokana na hilo, Morad, ambaye aliitwa Taifa Stars enzi za Maximo alipokuwa akiichezea Ashanti, ameshauri pia hata wanaochagua timu za taifa, makocha na viongozi, walenge timu za mikoani.

Mafanikio yake.

Ameeleza pia mafanikio yake yanatokana na kutobweteka. Anajituma sana ili kuona anafikia malengo anayotaka na mpango wake atoke nje ya nchi siku za usoni.

Anahusudu zaidi kuchezea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo au timu za Afrika Kusini.

Tofauti ya Azam FC na Kagera Sugar

"Klabu hizi zina tofauti kubwa ya maslahi, zote ni kampuni, lakini zinazidiana maslahi, lakini pia maadili na mazingira ya timu ni tofauti," anasema Morad.

"Ukiwa Kagera maisha ya kule ni magumu, kuanzia mnapoanza ligi hadi kumalizika. Ukiwa na roho ndogo maisha lazima yatakushinda. Hali hiyo inawafanya muda wote mnakuwa tayari kwa lolote, lakini hapa ni raha tu, tena ninacheza nikiwa nyumbani, muda wote ninaiona familia."

"Tukiingia kambini ni siku chache tu na baada ya mechi tunakuwa huru. Sasa ni suala la mwenyewe kuwa na nidhamu."

Stewart Hall

"Stewart ni kocha ninayemwamini na amenifanyia mengi. Kwa kweli makocha wa kigeni wana ujuzi wa hali ya juu, yaani siamini kama nimweka benchi mtu kama Nafiu, ambaye ni mchezaji wa kulipwa kutoka nje ya nchi," anasema Morad.

Taifa Stars na Azam FC

"Natamani nicheze Taifa Stars na ninaamini muda ukifika nitapata nafasi. Sawa waliopo Stars ni bora, lakini kama nitachaguliwa nitafanya mambo makubwa," aliongeza kusema Morad, ambaye pia aliwahi kuchezea Simba.

Kuhusu Azam, Morad anasema malengo yake ni kuisaidia kutwaa nafasi ya pili au kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara.

Morad anaamini kwa mshikamano walionao kikosini utawawezesha kutimiza malengo yao.

Historia

Morad, asili yake ni Pemba, Zanzibar, wanakotoka wazazi wake. Lakini yeye ni mzaliwa wa Dar es Salaam.

Katika familia anayotoka, wamezaliwa watoto saba na yeye ndiye kitinda mimba. Dada yake Hanifa ni marehemu na sasa amebaki yeye na ndugu wengine Morad, Dirishad, Khadija, Mgeni na Faudhia.

Kwa upande wake, ameshaingia katika maisha ya ndoa akiwa ni mume wa Fatna Yusuph, lakini hawajafanikiwa kupata mtoto.

Alianza kucheza soka wakati akisoma katika Shule ya Msingi ya Amana B Punje alikocheza mashindano ya Umitashumta.

Baada ya kumaliza shule alizichezea timu za mtaa wake za Shauri Moyo na African Stars zilizokuwa zinashiriki Ligi Daraja la kwanza.



Mwanaspoti

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.