Saturday, December 24, 2011
Jembe toka Ruvuma anaeiwakilisha Zanzibar Heroes
Posted By: kj - 11:43 AMDORIS MALIYAGA
HANA mafanikio makubwa labda kwa vile ameanza kung'ara katika miaka ya hivi karibuni tu. Lakini Aggrey Morris Ambrose, anayeichezea Azam FC, ni miongoni mwa mabeki bora nchini.
Umahiri wake umemfanya awemo kwenye kikosi cha kwanza cha timu ya taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes.
Ni beki ambaye hakuwahi kubweteka kwa sifa, ametulia, anajua anachotakiwa kufanya kwa wakati mwafaka na ana malengo ya sasa na siku zijazo.
Beki huyo wa kati, anayezimudu namba nne na tano kwa ufasaha, huwa hapendi kuremba na mpira. Anachojua ni kuchukua mpira kutoka kwa adui, kuutuliza na kutoa pasi sahihi.
Aggrey ni nani
Aggrey anaichezea Zanzibar Heroes akiaminika ni mwenyeji wa visiwani humo, lakini asili yake ni Tanzania Bara, mkoani Ruvuma. Wazazi wake wote wawili, wanatoka kandokando mwa Ziwa Nyasa katika Kijiji cha Manda.
Baba yake (Morris Ambrose) pamoja na mama yake (Esther Salvis), walihamishia makazi yao Zanzibar kwa shughuli za kikazi mwaka 1977 wanakoishi hadi sasa.
"Zanzibar sisi ni wahamiaji tu. Ila mimi nimezaliwa na kukulia visiwani humo (alizaliwa Machi 12, 1986), nimesoma Zanzibar na hata sasa makazi yangu yako huko," anasema Aggrey.
Anakiri kuwa aliwahi kwenda kijijini kwao kwa asili mara moja tu, lakini mama yake ndiyo huwa anaenda mara kwa mara.
"Nachezea Zanzibar Heroes kwa sababu nimetambulika kisoka nikiwa Zanzibar, sina sifa ya kuichezea Bara hata kama wazazi wangu ni wa kutoka huko," anasema beki huyo muumini wa Kanisa la Walokole ambaye ni shabiki mkubwa wa Arsenal.
Mafanikio yake
"Ninafanya vizuri kwa sababu najituma, mara zote huwa napenda kujifunza mambo mengi kutoka kwa wenzangu na hasa walionizidi kiwango," anasema.
"Ndiyo maana nasonga mbele. Lakini pia ninafanya mazoezi kwa nguvu, namsikiliza kocha na kufuata maagizo yake."
Simba na Yanga
Klabu za Simba na Yanga mara nyingi zimekuwa zikifika dau na kuchukua wachezaji wa klabu nyingine ambao huonekana kufanya vizuri.
Kwa upande wake anasema: "Sina mawazo ya kwenda Simba au Yanga, mimi ni mchezaji na kwa sasa nipo Azam FC, hicho ndiyo ninachojua. Muda wa kuondoka ukifika nitaangalia maslahi ya kazi kwani soka ndiyo kazi yangu. Nikiwa huru kutoka Azam kanuni zitaniongoza kwa kwenda kulingana na maslahi."
Soka la Klabu na Zanzibar
Anasema katika klabu yake ya Azam wamekutana wachezaji wanaotaka kuipa mafanikio makubwa timu hiyo ili kuandika historia mpya ya soka ya Tanzania.
"Unajua hapa watu wamezoea habari ya Simba na Yanga, sasa tunataka kushika nafasi za juu kama si kutwaa ubingwa, tutaweza," anasema.
Kuhusiana na Zanzibar Heroes na hasa ushiriki wake duni kwenye Kombe la Chalenji hivi karibuni, alikiri kukosa furaha lakini akisema watakuwa wameimarika zaidi mwakani.
Urojo
Mara nyingi mashabiki wa soka huwatania wachezaji wa Zanzibar kuwa ni urojo wakidaiwa kukosa ukakamavu, Urojo ni chakula maarufu visiwani humo.
Alipoulizwa hilo, Aggrey, kwanza alicheka, kisha akajibu akisema: "Hayo ni maneno tu, wala hayana mashiko. Katika soka ya Tanzania kwa sasa, kuna wachezaji mahiri tegemeo kutoka Zanzibar. Kuna mimi, yupo Nadir Haroub Canavaro kuna Nassor Said Cholo, pia wapo akina Abdulhalim Humoud na Abdi Kassim 'Babi', hivi hao unaweza kuwafananisha na urojo? Hizo ni porojo tu."
Historia
Katika familia anayotoka, Aggrey, ni wa nne kuzaliwa kati ya watoto watano. Kuna wanaume wengine wawili (Renatus na Aevis) na dada zao ni Austeria na Herena.
Akizungumzia historia yake ya soka, anasema alianza kucheza tangu utotoni mwake alipokuwa akisoma Shule ya Msingi Jang'ombe.
Mbali ya shuleni, mtaani alikuwa akiichezea klabu ya Siko tangu mwaka 2001. Mwaka 2004 aliteuliwa katika kikosi cha timu ya taifa ya vijana ya Zanzibar, Karume Boys iliyoshiriki Chalenji ya vijana, alikuwa nahodha.
Baada ya hapo alichukuliwa na klabu ya Mafunzo ya Ligi Kuu visiwani humo, kabla ya kuhamia Azam.
AGGREY MORRIS AMBROSE
Amezaliwa: 03. 12. 1986
Mahali: Jang'ombe, Zanzibar
Klabu: Siko 2001-2004, Mafunzo 2004-2009, Azam FC 2009-
Timu za Taifa: Karume Boys, Zanzibar Heroes na Taifa Stars
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
SIB 90
POPULAR
TAGS
0 Maoni:
Post a Comment