Saturday, December 17, 2011
Wachezaji wapya wampa hauweni Hall
Posted By: kj - 2:14 PMMUIVORY Coast Kipre Bolou, Gaudence Mwaikimba na Abdi Kassim Babi wamemtia wazimu Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall akikubali viwango vyao na kusema mambo poa, sasa ni mabao kwenda mbele.
Nyota hao wamesajiliwa katika usajili wa dirisha dogo ili kuongezea makali safu ya ushambuliaji ambayo kocha huyo raia wa Uingereza, alikiri ilikuwa ni tatizo kubwa katika mzunguko wa kwanza.
Bolou pacha wa Kipre Tchetche, amesajiliwa kutoka Hire ya Ivory Coast, Babi kutoka Dong Tam Long An ya Vietnam na Mwaikimba kutoka Moro United ambao wameungana na Joseph Owino kutoka Uganda ambaye sasa ni majeruhi.
Nyota hao wote kasoro Owino, wataanza kuonyesha makali yao, katika mechi ya Jumanne ijayo ya kirafiki dhidi ya Yanga Uwanja wa Taifa na baada ya hapo kwenye Kombe la Mapinduzi.
Akizungumza na Mwanaspoti Stewart alisema: "Wachezaji hawa, watatuliza moyo wangu, sikufanya vizuri sana mzunguko wa kwanza kwa sababu ya uhaba wa mabao, nilikuwa na washambuliaji na viungo wazuri, lakini tatizo hawafungi.
Ukiangalia viungo kama Redondo (Ramadhani Chombo), Salum Aboubakary (Sure Boy), Ibrahim Mwaipopo na wengine, lakini angalia wote wamefunga bao moja tu lile la Redondo, ndiyo sababu ya kuwaita hawa kwa sababu viwango vyao ni tofauti na sifa zao ni pekee wao, wanafunga.
Aliongeza kuwa: Nimemchukua Mwaikimba pia, tatizo ni hilo hilo la mabao, ukiangalia safu hiyo ni Boko (John Boko) pekee ndiyo alikuwa akifunga mabao na Anko (Mrisho Ngassa) sasa kama ataungana naye, mambo yatakuwa mazuri kwa sababu amekuwa akifanya vizuri na hata mzunguko wa kwanza.
Simba ndiyo inayoongoza Ligi Kuu ikiwa na pointi 28 ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 27, Azam 23 na Oljoro JKT 23.
mwanaspoti
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
SIB 90
POPULAR
TAGS
0 Maoni:
Post a Comment