Tuesday, January 3, 2012

Chaguo la kwanza Azam

Posted By: kj - 7:16 PM

Share

& Comment


DORIS MALIYAGA

KIPA Mwadini Ally, ameonyesha uwezo mkubwa ambao umemfanya kuwa miongoni mwa makipa bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa sasa.

Amejizolea sifa kwani amemkimbiza kipa wa kwanza wa Azam, Mserbia Obren Curkovic, ambaye amekwenda zake Vietnam.

Mwadini siyo mzoefu sana katika ligi hiyo, amecheza mechi 10 tu, lakini anafanya vizuri kama vile amekuwa kwenye ligi hii kwa muda mrefu.

Mwadini, ambaye amepata umaarufu na kuwa simulizi katika mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo, hana umbo kubwa kama walivyo makipa bora duniani, umbo lake ni la wastani. Kipa huyo ana sifa ya wepesi na usugu awapo langoni na kudhibiti vizuri timu pinzani.

Mwadini huwa haogopi shambulizi la aina yoyote linalotokea langoni mwake, lakini pia huwa mtulivu anaposhambuliwa. Uwezo wake huo, umefanya aaminiwe na makocha wake na kuwa kipa wa kwanza katika kikosi cha Zanzibar Heroes na Azam FC na sasa amepania kuwa kipa namba moja wa Taifa Stars.

Ameng'ara zaidi katika mzunguko wa kwanza akifanikiwa kumweka benchi Cirkovic. Kutokana na umahiri wa Mwadini, Mwanaspoti ilizungumza naye na kufahamu siri ya mafanikio yake na malengo yake katika soka.

Mafanikio na malengo Mwadini anasema kuwa mafanikio yake ni kutokana na kujituma na anafanya hivyo kwasababu hiyo ndiyo kazi yake. "Kujituma na kufuata maagizo ya kocha huenda ndiyo sababu inanifanya nifanye vizuri," anasema Mwadin ambaye anapenda soka la Lionel Messi wa Barcelona.

Kuwepo kwangu golini mara kwa mara, ni uamuzi wa kocha (Stewart Hall) na si mimi binafsi, hiyo ni kutokana na bidii ninayoonyesha mazoezini. Lakini pia ninafanya hivi nikiwa na malengo ya muda mrefu, kuhakikisha nasonga mbele na kuwa mchezaji wa kimataifa.

Kufanikisha hilo, anasema anajitahidi pia kuishi kwa nidhamu ya kiuanamichezo hasa katika muda wa mapumziko akiutumia kutulia nyumbani kuangalia televisheni na kusikiliza muziki.

Ushindani wa namba

Amekuwa na washindani wa namba katika kikosi cha Azam, Zanzibar Heroes na Taifa Stars. Azam ilikuwa na Cirkovic, ambaye kwa sasa ameihama timu hiyo.

Mwadini alifanikiwa kumweka chini na kudaka mechi 10 kati ya 13 za mzunguko wa kwanza. Kusimama kwake imara, kuliifanya Azam imalize mzunguko huo, ikiwa ya tatu, nyuma ya Simba na Yanga.

Lakini pia, akiwa ni kipa mpya wa Taifa Stars ana kibarua kigumu cha kumng'oa Juma Kaseja sambamba na Shaaban Hassan Kado na Shaaban Dihile ili kudumu katika kikosi hicho.

Mwadini, hata hivyo, anasema: Kila kitu ni malengo, kwanza unatakiwa kuwa mvumilivu, lakini pia kujifunza, huwezi kuanza moja kwa moja ukawa kileleni. Lazima kuanzia chini ndipo uende juu, sasa nasubiri na kama ni bahati yangu, muda utafika nitaongoza jahazi.

Mwadini alieleza furaha yake alipoitwa Taifa Stars, anasema ilikuwa furaha isiyo kifani kwani ilikuwa njia nyingine ya kukamilisha malengo yake ya kutamba katika soka ya kimataifa.

Azam na Stewart

Azam ni klabu nzuri na bora, kwani humfanya kila mchezaji kufanya kazi yake kwa ufasaha, anaeleza Mwadin aliyeweka wazi kuwa, mechi alizocheza akiwa na Zanzibar Heroes ndizo zilizomng'arisha.

Tunaishi vizuri kwa ushirikiano na kila mmoja anajua nini anafanya.

Naamini kama tutaendelea na kasi hii, tutafikia pazuri na kukamilisha malengo yetu ya kumaliza katika nafasi ya kwanza au ya pili.

Akimzungumzia kocha Stewart anayemfundisha akiwa na Azam na Zanzibar Heroes, Mwadini anasema ni babu kubwa.

"Yaani kocha Stewart, ndiyo kila kitu katika mafanikio yangu haya ya soka," anasema.

Amenifundisha mambo mengi ambayo awali nilikuwa siyajui, lakini sasa nimekuwa fundi. Nimekuwa najiamini tofauti na zamani, kiufundi ndiyo usiseme.

Simba na Yanga

Mimi ni mchezaji, nacheza mpira kwa ajili ya kuendesha maisha yangu, sasa kama hizo klabu za Simba na Yanga zina malengo nami, zikamilishe taratibu, nitazichezea, alisema Mwadini, ambaye alisajiliwa na Azam kwa mkataba wa miaka miwili.

Historia

Mwadini ni mtoto wa kwanza kuzaliwa katika familia ya watoto sita, wawili wakiwa wa kike ambao ni Mwantumu na Zuwena. Ndugu zake wengine ni Makame, Maulid na Mskena.

Kipaji chake cha soka, kilianza akiwa mtoto na kilipata umaarufu akiwa Shule ya Msingi Mkwajuni na alipomaliza alisajiliwa na timu ya Chongoi, yenyewe ilikuwa ikishiriki, Ligi Daraja la Pili.

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.