Sunday, March 11, 2012
Azam waweka rikodi 4
Posted By: kj - 3:51 PMJohn Bocco akishangilia goli lake la kwanza, akiambatana na wachezaji wenzake
IKITAFUTA rekodi mbili za klabu, Azam FC jana imejikuta ikipata rekodi nne kwa mpigo baaada ya kuisasambua Yanga 3-1 katika mchezo mkali wa ligi kuu ya Vodacom.
Rekodi ya kwanza imewekwa na mshambuliaji John Bocco ambaye leo amefunga magoli mawili na kufikisha jumla ya magoli 15 baada ya kushuka dimbani mara 18. Rekodi yake ni magoli 14 Msimu wa 2009/2010.
Endapo Bocco atafunga magoli mawili tuu kwenye mechi sita zilizosalia basi ataweka rekodi ya Klabu ambayo inashikiliwa na Mrisho Ngasa aliyefunga magoli 16 msimu uliopita. Ngasa hivi sasa ana magoli mawili tuu.
Rekodi ya juu ya magoli ligi kuu inashikiliwa na Boniface Ambani na Mussa Mgosi ambao waliwahi kufunga magoli 18.
Rekodi ya pili kwa Azam FC ni kufikisha pointi 41 kwenye ligi kuu tena ikiwa imecheza mechi 20 tuu. Azam FC ambayo huu ni msimu wake wanne kwenye ligi kuu haijawahi kufikisha pointi 41 katika historia yake tangia ianzishwe.
Katika msimu wake wa kwanza wa ligi kuu msimu wa 2008/2009. Azam FC ilimaliza na pointi 24, Msimu uliofuata wa 2009/2010 Azam FC ilimaliza ligi ikiwa na pointi 34 na msimu uliopita wa 2010/2011 Azam FC ilimaliza ligi na pointi 40.
Ukiangalia rekodi utaona kuwa timu imekuwa ikiimarika taratibu na msimu huu kitendo cha kufikisha poiti 41 huku ligi ikiwa bado inaendelea kimetoa matumaini makubwa sana.
Rekodi ya tatu ni kuifunga Yanga mara nne mfululizo. Rekodi hii imeanzia kwenye ushindi wa 1-0 kwenye raundi ya kwanza VPL na ikafuatia ushindi wa 2-0 kwenye mechi ya kirafiki ya Hisani kabla ya kuitandika Yanga 3-0 na kuisukumiza nje kwenye mashindano ya Mapinduzi cup.
Yanga walikuja kwenye mechi hiyo ya jana wakijigamba kuwa wao ndiyo wenye ligi na lazima waifunge Azam FC kwenye mechi ya jana na kuthibitisha kuwa wao sio tu mabingwa wa Afrika Mashariki na kati bali pia ni mabingwa Tanzania lakini hali ilikuwa tofauti baada ya kupokea kichapo cha 3-1.
Rekodi ya nne ni kuongoza ligi hata kama Azam FC imecheza michezo miwili zaidi ya Yanga na Simba. Tangia Azam FC ianzishwe, haijawahi kuongoza ligi wakati ligi imeingia raundi ya pili kwa namna yoyote ile. Hii ni rekodi kwa Azam FC na kutokana na kubanana kwenye nafasi ya juu.
Ligi ya Tanzania inakuwa na ushindani na mwamko mzuri zaidi ya ilivyokuwa huko nyuma.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Maoni:
Post a Comment