Sunday, April 15, 2012

Azam watoa kichapo Dodoma

Posted By: kj - 1:07 AM

Share

& Comment


Jitihada na uwezo wa wachezaji wa Azam FC umepelekea timu hiyo kupata pointi tatu muhimu baada ya kuifunga Polisi Dodoma 1-0 katika mchezo wa ligi kuu uliochezwa Jumamosi uwanja wa Jamhuri.

Mchezo wa jana ambao ulikuwa wa Upande mmoja kutokana na Polisi kuamua kupaki basi na kuzuia tuu kuanzia dakika ya kwanza huku wakipoteza muda kijinga kiasi cha kukera.

Azam FC wakiwa ugenini wamepata pointi hizo tatu na kufikisha jumla ya pointi 50 sawa na timu ya Simba wakitofautiana idadi ya magoli, kwa matokeo hayo Azam watakuwa wameiacha Yanga kwa pointi saba kabla ya michezo ya leo Jumapili.

Mchezo huo uliokuwa muhimu kwa Azam, ulianza kwa kasi katika dakika ya kwanza mchezaji Mrisho Ngasa wa Azam alishindwa kumalizia kazi nzuri ya Kipre Tchetche.

Kasi ya mchezo huo ilizidi kuongezeka Azam FC wakicheza katika kiwango cha juu japokuwa uwanja ulionekana kuwasumbua walitengeneza nafasi nyingi na kupelekea timu ya Polisi kuwachezea vibaya ''rafu' wachezaji wa Azam FC.

Kipindi cha Pili kilikuwa kigumu kwa timu zote, Polisi walionekana kuridhika na sare lakini Azam walihitaji ushindi ambao ungewaweka vizuri katika harakati za kusaka nafasi mbili za juu ikiwemo ubingwa.

Goli la Azam limepatakana katika dakika ya 79 kupitia kwa nahodha Agrey Moris baada ya kupigwa mpira wa kona ukaokolewa na mabeki wa Polisi na kutua kwa Agrey aliyeandika goli hilo pekee na la ushindi kwa Azam.

Polisi watajutia kitendo cha kupoteza muda katika mchezo huo, baada ya mchezaji Bakari Nzige kutolewa kwa kadi nyekundu na mwamuzi Martin Saanya kwa kosa la kupoteza muda, Nzige ameonyeshwa kadi mbili za njano ya kwanza ilikuwa kipindi cha kwanza alipomfanyia madhambi Kipre wa Azam na ya pili kwa kupoteza muda.

Azam walifanya mabadiliko walitoka Jabir Aziz dk 59 akaingia Khamis Mcha, dakika ya 72 akatoka Mrisho Ngasa nafasi yake ikachukuliwa na Mwaikimba.

Baada ya kumalizika kwa mchezo huo, mwamuzi Saanya alivamiwa uwanjani na mashabiki wa Yanga na Simba waliojivika ngozi za timu ya Polisi na kuokolewa na maaskari, lakini kitendo cha kuhuzunisha kilitokea katika vyumba vya kubadilishia nguo mwamuzi huyo alipigwa sehemu za usoni na mashabiki hao mamluki wa Polisi Dodoma hali iliyopelekea kutokwa na damu.

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.