Monday, December 10, 2012

AZAM; SOMBA WA:ITANGULIA KUVUNJA MKATABA

Posted By: kj - 9:29 AM

Share

& Comment



Na Mahmoud Zubeiry
 
KLABU ya Azam FC imesema kwamba, Simba SC ilikiuka mkataba wao wa kuwauzia kwa mkopo mchezaji Mrisho Ngassa kwa kitendo cha kumsainisha mkataba nyota huyo na kumpa gari aina ya Verosa na Sh. Milioni 18.
 
Taarifa ya Azam kwa BIN ZUBEIRY, imesema kwamba, wanashangaa Simba kulalamikia Azam kumuuza El Merreikh ya Sudan bila ya kufikia nao makubaliano, wakati wao walianza kukiuka mkataba. 
 
“Kwanza tunapenda umma uelewe kwamba, sisi tuliwashirikisha Simba mapema tu katika mpango huu, lakini wao wakataka fedha nyingi, ambazo Merreikh hawakuwa tayari kutoa, na sisi kwa kuzingatia maslahi ya mchezaji na taifa, tukaamua kutumia haki yetu, akiwa mchezaji wetu kwa kuamua kumuuza,”imesema taarifa ya Azam.
 
Azam imeliandika barua Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) juzi ikiwaomba wamruhusu Ngasa kwenda Sudan kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya afya katika harakati zake za kujiunga na El Merreikh ya nchini humo.
 
Azam FC imesema kwamba, katika barua waliyowapelekea TFF, nakala wamewapelekea pia na Simba SC, ambako mchezaji huyo alikuwa anacheza kwa mkopo.
 
“Msukumo uliotufanya tuandike barua hii ni kwa kutambua kuwa hii ni nafasi muhimu kwa Ngassa na taifa, kwani anakwenda kucheza kwenye timu yenye uwezo na miundombinu mikubwa barani Afrika, na inayoshiriki ligi ya mabingwa Afrika karibu kila msimu, kitu ambacho kitamuongezea Ngassa kiwango na kuwa na msaada kwa tafa,”ilisema taarifa ya Azam.
 
Aidha, Azam wamesema pia wanapenda kuweka wazi thamani ya usajili na mshahara ambao Ngassa. Wamesema Ngassa atakuwa anapewa na El Merreikh mshahara wa dola za Kimarekani 4,000, kiasi cha Sh. Milioni 6 za Tanzania kwa mwezi, ambazo kwa miaka miwili ni takribani Sh. Milioni 144 Milioni.
Wamesema mchezaji huyo amepewa fedha za kusaini dola za KImarekani 50,000, kiasi cha Sh. Milioni 80.
 
“Kwa hiyo Ngassa ataweka kibindoni zaidi ya Shilingi Milioni 230 kwa miezi 24, hizi ni fedha nyingi kwa mchezaji wa kitanzania na kwa maendeleo ya mchezaji na familia yake na yatawapa msukumo vijana wengi wenye kipaji kama Ngassa kufanya bidii kwenye soka na kuliletea maendeleo taifa,”ilisema taarifa ya Azam.
 
Azam FC imeomba TFF imruhusu Ngassa kwenda Sudan akitokea Uganda kwenda kukamilisha vipimo vya Afya na usajili na Azam FC ipo tayari kukaa na Simba na kuzungumza juu ya uhamisho huu kwa usimamizi wa TFF.
 
"Hapa ieleweke kuwa ingawa Azam FC inajua haki zake kisheria, lakini pia imeamua kupunguza msimamo wake kukubali mazungumzo kwa kuangalia zaidi athari ambazo mchezaji anaweza kupata kimaslahi na kimaendeleo ya uchezaji wake na mpira wa Tanzania kwa ujumla kutokana na mgogoro huu,”iliongeza taarifa hiyo.
 
Lakini Makamu Mwenyekiti wa Simba SC, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ amesema klabu yake haiko tayari kufanya mazungumzo na Azam FC juu ya suala hilo.
 
Kaburu amesema, klabu yake iliingia mkataba na Azam FC kwa kununua haki zote za huduma za Ngassa kwa mwaka mmoja, hadi Mei 21 mwakani, ikilipa Sh. Milioni 25 kama ada ya kumtumia mchezaji huyo kwa mwaka mmoja pamoja na kumlipa mchezaji haki zake zote stahiki za kimkataba ikiwemo mshahara wake.
 
Kaburu amesema Azam bila ya kuzingatia mkataba iliousaini na Simba SC, na matakwa ya FIFA yanayohusu mkopo, iliamua kutangaza kumuuza Ngassa bila ya kuihusisha Simba wakati ikijua kuwa ilikuwa na Mkataba na Simba SC ambayo ameishaichezea katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Bara.
“Kitendo cha Azam FC kuongea na Klabu ya El Merreikh FC na kuweka makubaliano ya mauzo ya mchezaji na kumtangaza kuwa kimemuuza mchezaji Ngassa bila ya kuihusisha Simba SC, na baadaye kuiandikia klabu ya Simba kuwa kimeamua kumrudisha mchezaji Ngassa Azam, wakati ikijua kuwa ina mkataba na Simba SC ni uvunjifu mkubwa wa taratibu na umeleta athari kubwa kwenye klabu yetu,”alisema Kaburu na kuongeza;
 
“Tayari Simba SC ilikwishatuma malalamiko TFF na kupeleka pingamizi lake juu ya sulala hili kwa Rais wa TFF, Leodegar Tenga, ambapo imeamuliwa kuwa suala hili liende kwenye Kamati ya Sheria, Katiba na Hadhi ya Wachezaji likapatiwe ufumbuzi,”alisema.
 
Amesema Simba imekuwa ni klabu yenye kuangalia zaidi maslahi ya wachezaji na haina kipingamizi kwa kuwaruhusu wachezaji wake kutoka pindi wanapopata timu nje ya nchi kama utaratibu unafuatwa.
 
Kaburu amesema Simba SC ilikuwa tayari kukaa mezani na Azam kwa mazungumzo, lakini kwa kuwa Azam haipo tayari kutambua haki za Simba SC na imekuwa ikilitekeleza suala hili kiholela, hivyo haioni sababu za kuzungumza na Azam FC na kuliacha suala hili liende kwenye Kamati ya Sheria, Katiba na Hadhi ya Wachezaji kama TFF ilivyoagiza.


Source; BIN ZUBEIRY

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.