Omong alitua Dar es Salaam juzi Jumamosi
akiongozana na mtoto wake wa kwanza, Erick, ambaye ndiye meneja wake na
leo Jumatatu ndiyo anaanza kazi.
Kocha huyo amesisitiza kuwa amekuja Tanzania
kufanya mambo matatu ambayo ni lazima ayakamilishe ndani ya mwaka mmoja;
la kwanza ni kuipa Azam ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, pili ni
kuandika historia mpya kwa kufanya vizuri Kombe la Shirikisho na tatu ni
kuwaendeleza vijana wa Azam Academy.
Malengo ya kocha huyo yanawapa matumaini mabosi wa
Azam ambao kupitia Makamu Mwenyekiti wao, Said Mohamed, wamempa hadhi
ya kuwa ‘Bingwa wa makocha’.
Hiyo ni kutokana na historia yake ya nyuma
alipokuwa na A.C Leopards ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Brazaville
ambayo ilikuwa haijapata upingwa wa ligi kwa miaka 30.
Alitumia utaalamu wake katika kuipa timu hiyo
mafanikio kwani walitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Congo Brazaville kwa misimu
miwili mfululizo wa 2012 na 2013.
Kubwa zaidi ni pale A.C Leopards ilipotwaa ubingwa
wa Kombe la Shirikisho Afrika mwaka jana, na mwaka huu Leopards
ilitolewa kwenye hatua ya makundi kwa michuano ya Ligi ya Mabingwa
Afrika.
Anakuwa kocha wa tano wa kigeni kuifundisha Azam
baada ya Wabrazili, Neider dos Santos na Itamar Amorin. Wageni wengine
waliopita hapo ni Stewart Hall (Mwingereza) na Boris Bunjak (Mserbia).
Mwanaspoti ilipofanya mazungumzo na kocha huyo
kupitia ukalimani wa mwanaye, Erick, anayeweza kuzungumza Kiingereza kwa
ufasaha, kocha huyo anayezungumza zaidi Kifaransa anasema: “Mtazamo
wangu uko mazoezini, huko ndiko nitaangalia namna gani tutafanikiwa na
siyo jambo lingine, nahitaji kukaa na wachezaji ili kuwafahamu vizuri na
jinsi watakavyokamilisha malengo yangu.
“Nimekaa na uongozi kwa muda, tukazungumza na
kukubaliana, najua malengo ya timu ambayo ndiyo nitayafanyia kazi.
Naahidi kuwapa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu, kufanya vizuri na
kuandika historia katika michuano ya Kombe la Shirikisho pamoja na
kuendeleza Academy ya klabu.”
Kuhusiana na kuikuta ligi katikati huku yeye akiwa
hana uzoefu wa soka la Tanzania, alisema: “Nitafanikisha malengo yangu
kwani sioni sababu ya kushindwa.”
Omong anasema, anafahamu Azam ni timu kubwa na
aliifahamu iliposhiriki Kombe la Shirikisho Afrika kabla ya kutolewa na
Wamorroco (AS FAR RABAT). Anasema anafahamu timu hiyo iliitoa Al Nasir
Juba ya Sudan Kusini kwa jumla ya mabao 8-1 na Barack Young Controllers
II ya Liberia kwa jumla ya mabao 2-1.
Simba na Yanga/Lugha
Klabu za Simba na Yanga ndiyo kongwe na maarufu nchini, lakini Omong anasema hazifahamu kabisa klabu hizo.
“Sizijui Simba wala Yanga, lakini mimi ni kocha mwenye filosofi yangu, sioni kama itakuwa shida kwangu,”anafafanua.
Akizungumzia lugha anasema: “Sijui Kiswahili,
najua Kiingereza kidogo, Kifaransa ndiyo lugha yangu. Lakini sidhani
kama kutakuwa na tatizo katika kuwasiliana na wachezaji kwa sababu mpira
ni ufundi na unazungumza lugha moja.”
Wasifu wake
Omong ana umri wa miaka 63. Wakati uchezaji wake,
alicheza nafasi za beki wa kati na kiungo mkabaji. Ana watoto wanne
wakiwamo wawili wanawake, Erick ndiye wa kwanza.
Ni mchezaji wa zamani wa Dragon Yaounde ya
Cameroon. Alijifunza ualimu wa michezo na elimu ya viungo katika Chuo
cha Higher Institute of Youth and Sports kilichopo Yaounde, Cameroon.
Mwaka 1987 alipata Stashahada ya Ukocha wa Soka na
leseni B ya ukocha kwa viwango vya Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa),
alipata baada ya mafunzo yaliyofanyika Ujerumani.
Akiwa kwao Cameroon, Omong alizifundisha klabu za
Fovu of Baham na Ainglwe of Menoua ambayo ilifuzu fainali za Kombe la
Cameroon.
Mwaka 2001 alikuwa Kocha Msaidizi wa timu ya Taifa
ya Cameroon ‘Indomitable Lions’ chini ya Mjerumani, Winfried Schafer na
mwaka 2010 aliinoa timu ya Taifa ya Cameroon kwa wachezaji wa ndani
kabla ya kutimkia Congo.
Omong sasa ndiye amebeba roho ya Azam. Ni wazi
timu hiyo imepata kocha mwingine bora mwenye uzoefu wa kufanya kazi na
wachezaji maarufu duniani kama vile Samuel Eto’o na Alex Song.
Lakini uongozi na wamiliki wa Azam wanapaswa kujua
kwamba kocha huyo atahitaji muda ili kuleta mafanikio Chamazi, hivyo
wanapaswa kuwa tayari kuwa na subira.
Vinginevyo itaendeleza wimbi lake la kuwabadilisha makocha.
Katika msimu wake wa kwanza ligi kuu, Azam ikiwa bado inaundwa na
wachezaji wengi waliopandishwa timu, ilimfukuza Santos baada ya kufungwa
na Simba SC.
Itamar aliondoka kwa sababu ya kuzidiwa nguvu na
wachezaji wasio na nidhamu mbele ya uongozi wakati Hall mara ya kwanza
aliondolewa tu katika mazingira ambayo hayakueleweka, walimchoka tu na
wakamwajiri Bunjak.
Mserbia huyo naye, pamoja na kuiongoza vizuri timu
ikiwa kwenye mbio za ubingwa hadi mwishoni mwa mzunguko wa kwanza,
baada ya kufungwa na Simba naye akafukuzwa. Akarudi Stewart na
akafanikiwa kuzifunga Simba na Yanga katika ligi msimu huu, lakini
haikutosha baada ya mzunguko wa kwanza, akaambiwa aondoke. Sasa timu iko
mikononi mwa Omong, tusubiri kuona atakachofanya.
CHANZO: MWANASPOTI
0 Maoni:
Post a Comment