Mabingwa watetezi wa kombe la mapinduzi, Azam FC pamoja na timu mbili za Uganda; KCC na URA sambamba na Simba SC wamefanikiwa kutinga nusu fainali ya mashindano ya kombe la Mapinduzi yanayoendelea Zanzibar baada ya kuwabwaga wapinzani wao kwenye michezo ya robo fainali iliyopigwa leo Unguja na Pemba.
Katika mchezo ulipigwa saa nane mchana, Azam ilikuwa ya kwanza kutinga nne bora baada ya kuwabwaga Cloves Stars ya Pemba kwa magoli 2-0 yote yakifungwa kipindi cha pili na walinzi Aggrey Morris na Waziri Salum.
Mchezo wa pili kwenye uwanja wa Gombani Pemba, watoza ushuru wa Uganda, URA wamewafyatua maafande/mabaharia KMKM kwa goli 1-0 la Owen Kasule dakika ya 42, kwa mkwaju wa chinichini baada ya walinzi kuzembea kuondoa mpira langoni.
Kwenye mchezo wa Unguja KCC wamefanikiwa kucheza nusu fainali wakiwatoa mashindanoni makamu bingwa wa mwaka jana Tusker ya Kenya katika changamoto ya mikwaju ya penati baada ya dakika 90 kumalizika huku timu hizo zikiwa 0-0.
KCC walifaniukiwa kuweka kimiani penati zao zote 4 wakati Tusker wakifunga tatu tu na moja ya Ismail Dunga ikiokolewa na mlinda lango Salim Magoola na ya Luke Ochieng ikigonga mlingoti wa goli
Katika mchezo huo Tusker walilazimika kucheza dakika nne za mwisho wakiwa 10 baada ya kiungo Osborne Monday kutolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kuoneshwa kadi ya pili ya njano.
Masuala mengine mawili muhimu ya mchezo huo ni la walinda milango wawili Ochieng na Magoola kupiga mikwaju yao ya penati kwa kufuatana na kufunga, na pia timu ya Tusker kumaliza dakika 90 bila kupiga hata mkwaju mmoja uliolenga lango huku KCC wakipiga mikwaju 5 langoni ambayo ama iliokolewa na kipa au kugonga mwamba.
Mchezo mwingine uliiochezwa katika Uwanja wa Amaan ulishuhudia Simba wakiibuka na ushindi wa magoli 2-0 ya Ramadhani Singano dakika ya 47 na Amissi Tambwe dakika ya 58.
Kwa matokeo hayo Simba wataikabili URA ya Uganda katika mchezo wa nusu fainali ya pili keshokutwa Ijumaa baada ya nusu fainali ya kwanza kati ya mabingwa watetezi Azam na KCC, michezo yote uwanja wa Amaan. Fainali ni Jumatatu Januari 13.
0 Maoni:
Post a Comment