Thursday, April 17, 2014

HII NDIO AZAM BWANA...

Posted By: kj - 4:55 PM

Share

& Comment

Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam  MWISHONI mwa wiki, Azam FC ilifanikiwa kujihakikishia taji la ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya kuifunga Mbeya City mabao 2-1 Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.  Azam imefikisha pointi 59 ikiwa na mchezo mmoja wa kufunga pazia la Ligi Kuu Jumamosi dhidi ya JKT Ruvu Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam na siku hiyo itawania kuvunja rekodi ya Simba SC na Pan Africans kutwaa ubingwa wa ligi hiyo pasipo kupoteza mechi. Waliokuwa wapinzani wao katika mbio za taji hilo, Yanga SC walioifunga 2-1 JKT Oljoro Jumapili mjini Arusha, wakiifunga na Simba SC keshokutwa watafikisha pointi 58.
Tunainua Kombe; Wachezaji wa Azam FC wakishangilia ushindi wa 3-0 dhidi ya Ruvu Shooting wiki iliyopita Uwanja wa Mabatini, Mlandizi, Pwani.
Pamoja na kuwa timu ya kwanza kuifunga Mbeya City kwenye Uwanja wake siku hiyo, Azam FC pia imekuwa timu ya kwanza nje ya Simba na Yanga kutwaa ubingwa wa Bara tangu mwaka 2000 Mtibwa Sugar ilipofanya hivyo. Azam inakuwa timu ya saba nje ya Simba SC kutwaa taji la Ligi Kuu, baada ya Cosmo mwaka 1967, Mseto mwaka 1975, Pan Africans mwaka 1982, Tukuyu Stars mwaka 1986, Coastal Union 1988 na Mtibwa Sugar mara mbili mfululizo 1999 na 2000. Azam inatwaa ubingwa huo katika msimu wake wa sita kushiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, tangu ipande msimu wa 2008/2009. Azam FC ilianzishwa na kikundi cha wafanyakazi wa kampuni ya Mzizima Flour Mill, kampuni tanzu ya Bakhresa, makao yake makuu yakiwa Barabara ya Nyerere, Dar es Salaam. Lengo la wafanyakazi hao wa kampuni inayomilikiwa na Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake, awali ilikuwa ni kucheza kwa ajili ya kujiburudisha, baada ya kazi. Lakini baada ya kuona wana timu nzuri, Oktoba 16, mwaka 2004, waliisajili rasmi kwa ajili ya kushiriki Ligi Daraja la Nne, wakitumia jina la Mzizima FC.  Baadaye Mkurugenzi Mkuu wa makampuni ya Bakhresa, Abubakar Bakhresa, aliona ni vyema timu hiyo ihusishe wafanyakazi wa kampuni zote za Bakhresa, na kutumia jina la moja ya bidhaa zao kubwa, Azam. Kampuni nyingine za Bakhresa ni Food Products Ltd, Azam Bakeries Ltd, Omar Packaging Industries Ltd, Azam Marine na kadhalika.  Wazo lake lilikubaliwa na wafanyakazi wa kampuni hiyo, ndipo timu hiyo ikaanza kuitwa Azam SC, badala ya Mzizima. Lakini baadaye Juni 11, mwaka 2007, ilibadilishwa jina tena na kuwa Azam FC.  Azam ilikwenda kwa kasi nzuri kuanzia Daraja la Nne na hadi mwaka 2008, ilifanikiwa kucheza Ligi Kuu, ikipandishwa na makocha King, aliyekuwa akisaidiwa na Habib Kondo. Baada ya kupanda, Azam ilimuajiri kocha wa zamani wa Simba SC, Mbrazil Neider dos Santos, aliyekuwa akisaidiwa na Sylvester Marsh na Juma Pondamali upande wa kuwanoa makipa.
Stewart Hall alijiuzulu Novemba mwaka jana
Baadaye ilimuongeza kocha wa viungo, Itamar Amorin kutoka Brazil pia, ambaye awali ya hapo alikuwa msaidizi wa Marcio Maximo katika timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars. Ilisajili pia wachezaji nyota, wazoefu, wakiwamo kutoka nje ya Tanzania, ambao walichanganywa na chipukizi wachache walioipandisha timu hiyo, kama John Bocco ‘Adebayor’. Wakati Azam inapigana kwenye Ligi Daraja la kwanza ili kupanda Ligi Kuu, kikosini ilikuwa ina wakongwe kama Shekhan Rashid na Suleiman Matola, viungo wa zamani wa klabu ya Simba. Malengo makuu ya Azam ni kuifanya timu iwe ya kulipwa, wachezaji wakihudumiwa vizuri, chini ya makocha bora, nao waweze kufanya vizuri na kuitangaza kimataifa timu hiyo na soka ya Tanzania kwa ujumla. Aidha, kwa kuwa inataka kutambulika kimataifa, ina kitengo maalumu cha soka ya vijana, kilicholenga kuibua vipaji vya chipukizi wa soka na kuwakuza katika misingi na maadili ya mchezo wenyewe, ili baadaye wauzwe Ulaya. Mmoja kati ya mabosi wa Azam, Yussuf Bakhresa, ni wakala wa wachezaji anayetambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), ambaye anaweza kuwafanya yosso wa klabu hiyo waende Ulaya moja kwa moja. Kikosi cha kwanza cha Azam Ligi Kuu kilikuwa kinaundwa na wafuatao; Kassim Kilungo, Said Bakar Nachikongo, Abdul Azizi Hamza, Shaaban Abdallah Kisiga ‘Malone’, Ally Suleiman Alawy, John Raphael Bocco ‘Adebayor’, Salum Machaku, Shekhan Rashid Abdallah, Jamal Simba Mnyate, Yussuf Juma Gogo, Zuberi Ubwa, Yahaya Said Tumbo, Said Khamis Sued, Salum Abubakar Salum, Luckson Jonathan Kakolaki, Adam Shomari Ngido, Abdulhalim Chilumbe, Ngoy-Pichou Botwetwe, Mussa Khalid Kipao, Iddi Abubakar Mwinchumu, John Faustin Mabula, James Adriano Kilongola, Malika Philipo Ndeule, Paulo John Nyangwe, Boniface Pawasa na Vladimir Niyonkuru. Azam ni klabu mfano wa kuigwa nchini, ikiwa inamiliki Uwanja wake wa kisasa, Azam Complex sambamba na hosteli za kuishi wachezaji uliozinduliwa na rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete mwaka jana.  Uwanja huo uliweka rekodi ya kuwa Uwanja wa kwanza wa klabu nchini mwaka huu kutumika kwa michuano ya kimataifa. Azam wenyewe walicheza hapo mechi yao na Ferroviario ya Msumbiji katika Kombe la Shirikisho Afrika, wakati timu ya taifa ya wanawake, Twiga Stars ilicheza hapo na Zambia katika kuwania tiketi ya Fainali za Afrika za wanawake na timu zote zikatolewa katika hatua ya kwanza. Azam Complex yenye kila kitu cha kuifanya iitwe ya kisasa, ikiwemo gym, bwawa na kuogelea na viwanja vya ziada vya mazoezi, bado inaendelea kuboreshwa ili kuifanya iwe bora zaidi. Cha kujivunia zaidi ni akademi ya Azam Complex, ambayo baada ya muda mfupi matunda yake yameanza kuonekana. Tayari wachezaji wa akademi ya Azam ni msaada kwa timu ya wakubwa iliyotwaa ubingwa wa Ligi Kuu, hapo unawazungumzia vijana kama Aishi Manula, Bryson Raphael, Gadiel Michael, Kevin Friday, Farid Mussa, Joseph Kimwaga, Mudathir Yahya wote hao wana jasho lao kwenye ubingwa wa kwanza wa Ligi Kuu wa timu hiyo.  Azam FC ilikuwa inafukuzana na Yanga SC katika mbio za ubingwa na msimu huu imevuna pointi nne kati ya sita kutoka kwa mabingwa hao wa msimu uliopita na pointi hizo zilipatikana kwa jitihada za wachezaji waliopandishwa kutoka akademi iliyo chini ya mwalimu Vivek Nagul kutoka India akisaidiwa na mzalendo, Philipo Alando, mchezaji wa zamani wa timu hiyo.
Boris Bunjak kulia aliifundisha Azam katikati ya vipindi viwili vya Stewart Hall
Joseph Kimwaga alifunga bao la ushindi dakika za lala salama Yanga ikilala 3-2 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza Ligi Kuu na Kevin Friday akafunga bao la kusawazisha dakika za mwishoni katika sare ya 1-1 na Watoto hao wa Jangwani- huku kipa Aishi Manula akidaka vizuri mno pamoja na kuicheza penalti ya Hamisi Kiiza. Watoto wa akademi ya Azam tayari ni tegemeo la taifa, wamekuwa wakitawala katika timu za vijana kuanzia U17 na wameanza kupenya hadi timu ya wakubwa, Taifa Stars. Aishi, Ismail Gambo ‘Kussi’ ambaye baadye aliumia, Farid Mussa, Mudathir Yahya na Joseph Kimwaga wote waliitwa Novemba mwaka jana katika kikosi cha Stars na kocha aliyetupiwa virago, Mdenmark Kim Poulsen. Katika kikosi cha sasa cha U20 kilichopo kambini kwa ajili ya mchezo wa marudiano na Kenya wiki ijayo kuwania tiketi ya Fainali za Afrika mwakani nchini Senegal, Akademi ya Azam ina wachezaji 12 ambao ni Kevin Friday, Jamil, Farid Mussa, Mange, Masoud, Mudathir, Bryson Raphael, Swaleh, Dismuss, Gadiel Michael, Hamadi Juma na Aishi.  Katika kikosi kipya cha maboresho ya Taifa Stars, kinachohusisha wachezaji waliokusanywa baada ya mchakato wa kusaka vipaji nchi nzima, Azam akademi ina wachezaji wawili ambao ni Reyna Ally na Shiraz Abdallah katika kambi ya timu hiyo iliyopo Tukuyu mkoani Mbeya. Kwa hakika ni mafanikio makubwa kwa timu hiyo yenye nusu muongo tu katika Ligi Kuu ya nchi na ambayo Oktoba 16, mwaka huu itatimiza miaka 10 ya kuanzishwa kwake rasmi.
Gaudence Mwaikimba kushoto alifunga mabao muhimu katika mechi za mwishoni mwa msimu

SAFARI YA UBINGWA… Azam ilianzishwa kama timu ya wafanyakazi kujifurahisha na kutimiza kaulimbiu michezo ni afya, lakini baada ya wamiliki kuamua kuifanya kuwa timu rasmi, walijiwekea malengo, kwanza kupanda hadi kucheza Ligi Kuu na baadaye kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu- kisha kutwaa mataji ya Afrika, ili ifikie kuitwa klabu kubwa mfano wa nyingine barani, kama Al Ahly, TP Mazembe, Pirates na nyingineo. Mikakati na mipango mingi iliundwa ili kufanikisha malengo hayo, ikiwa ni pamoja na kuunda akademi, ambayo matunda yake yameanza kuonekana. Wapinzani wa Azam FC walitumia mamilioni kusajili mwanzoni na katikati ya msimu, wakati timu hiyo ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake ilipandisha wachezaji wa akademi zaidi. Agosti mwaka jana, Azam FC iliweka kambi ya karibu wiki mbili nchini Afrika Kusini kujiandaa na msimu ambako pamoja na kufanya mazoezi, ilicheza mechi ngumu za kirafiki za kujipima nguvu dhidi ya timu kubwa za huko. Azam ilianza ziara hiyo kwa kufungwa mabao 3-0 na Kaizer Chiefs, kabla ya kuifunga Mamelodi Sundwons 1-0 katika mchezo uliofuata, kisha kufungwa na Orlando Pirates 2-1 na kumalizia ziara kwa kipigo cha 1-0 cha Moroka Swallows. Kambi hiyo iliijenga mno Azam na japokuwa ilifikia kipigo cha 1-0 kutoka kwa Yanga SC katika mchezo wa Ngao ya Jamii, lakini wazi ilionekana waliathiriwa na mabadiliko ya hali ya hewa, kwa kuwa walirejea nchini siku mbili kabla ye mechi hiyo.
Matunda ya akademi; Kevin Friday akishangilia na Gardiel Michael baada ya kufunga bao la kusawazisha dhidi ya Yanga SC
Aliyekuwa kocha wa Azam FC wakati huo, Muingereza Stewart Hall alijiuzulu baada ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, na nafasi yake ikachukuliwa na Mcameroon Joseph Marius Omog ambaye ameifikisha timu kwenye ubingwa baada ya kuiongoza katika mechi 12 za ligi bila kupoteza hata moja, ikishinda mechi 10 na kutoa sare mbili. Kwa ujumla hadi sasa, Omgo ameiongoza Azam FC katika mechi  20 za mashindano yote, akiiwezesha kushinda mechi 16 kufungwa mbili sare mbili. Kwanza alifungwa 3-2 na KCC ya Uganda katika Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar na baadaye akafungwa 2-0 nchini Msumbiji na Ferroviario katika Kombe la Shirikisho.  Omog anakuwa kocha wa tano wa Azam FC tangu ianze kucheza Ligi Kuu, baada ya Wabrazil Neider dos Santos, aliyemuachia Itamar Amorin ambaye alikuwa msaidizi wake, Stewart Hall aliyempisha kwa muda Mserbia Boris Bunjak msimu uliopita kabla ya kurejea kumalizia mzunguko wa pili, na kuachia tena baada ya mzunguko wa kwanza msimu huu akimuachia Mcameroon huyo.    Haikuwa kazi rahisi kwa Azam FC kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu baada ya kuukosakosa kwa misimu miwili iliyopita. Ilipitia ligi ngumu, ya ushindani lakini ikasimama imara wakati wote hadi kutimiza malengo. Hongera Azam FC, sasa watu watapenda kuona mambo mazuri katika michuano ya Afrika.

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.