Wednesday, April 16, 2014

KUTETEA TAJI SI KAZI RAHISI

Posted By: Unknown - 12:29 PM

Share

& Comment

Meneja wa Azam FC, Jemedari Said
MABINGWA wapya wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara, Azam FC wamesema kutwaa taji si kazi ngumu kama kuendelea na wimbi la ushindi, changamoto ambayo inawakabili msimu ujao.

Azam FC imetwaa ubingwa wa kwanza katika historia ya soka Tanzania, ikiwa ni miaka sita baada ya kucheza Ligi Kuu. 

Ilianzishwa mwaka 2007.

Ilitwaa ubingwa huo uliokuwa ukishikiliwa na Yanga mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya kuifunga Mbeya City mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Akizungumza na gazeti hili jana, Meneja wa Azam, Jemedari Said alisema haikuwa kazi rahisi kutwaa ubingwa, lakini kazi inayowakabili mbele yao ni ngumu zaidi kuliko waliyokwishaifanya.

“Tumetwaa ubingwa, lakini tunaona haikuwa kazi sana kama kuendelea na mpango huo kuanzia msimu ujao. Je, tutaendelea kushinda na kutwaa ubingwa tena na tena? Hapo ndipo kwenye ugumu,” alisema Said.

Timu hiyo ya Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, imetwaa ubingwa ikiwa na mechi moja mkononi na ikishinda mechi hiyo, itafikisha pointi 62 na kuvunja rekodi ya Simba iliyowahi kutwaa ubingwa ikiwa na pointi 61.

“Tutavunja rekodi ya Simba ikiwa imetwaa ubingwa na pointi 61, lakini pia tunataka tufikie rekodi ya Arsenal ilitwaa ubingwa ikiwa imeshinda mechi 49, na sisi tunataka hivyo,” alisema mchezaji huyo wa zamani wa Kariakoo Lindi.

Kuhusu ushiriki wa michuano ya kimataifa, Said alisema wanasubiri ripoti ya kocha wao, Joseph Omog ndipo wajue wanafanya nini.

“Tunajua baada ya ubingwa kuna kitu kingine mbele yetu, nacho ni Ligi ya Mabingwa Afrika, je tutafika mbali kwenye michuano hiyo, isije kuwa tena mtoto akililia wembe mwache umkate… 

“Lengo la Azam ni kuwa klabu kubwa Afrika kama ilivyo TP Mazembe (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo), Ismailia, Zamalek (Misri) Esperance (Tunisia), ili tufike huko ni lazima tuwe mabingwa nyumbani, na ili tutimize malengo yetu sasa lazima tufanye vizuri Afrika…

 “Tunachosubiri kwa sasa ni taarifa ya kocha kuelekea kwenye michuano ya kimataifa… nani anamtaka, nani anaona hafai, anataka mchezaji kutoka wapi kuimarisha kikosi, anataka kwenda kucheza mechi za majaribio wapi kujiandaa na michuano ya Afrika, sisi tutamfanyia, lakini pia tutampa masharti yetu ya kile tunachokitaka,” alisema Meneja huyo wa Azam FC.

Tangu kupanda Ligi Kuu, Azam imeshiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika mara mbili baada ya kushika nafasi ya pili katika misimu miwili mfululizo, ingawa haikufanya vema katika michuano hiyo.

Lakini Said anasema wana imani na Omog kwa vile amekuwa kocha mwenye mafanikio Afrika.

“Sio kwamba hatumpi heshima yake kocha aliyepita (Stewart Hall) hapana, tunamheshimu sana, kwani mawazo yake tuliyafanyia kazi na sasa tunaona matunda yake. 

Yeye aliachia timu mzunguko wa kwanza ikiwa haijapoteza mechi, na Omog naye ameingia mzunguko wa pili naye hakupoteza mechi, kwa hiyo hawa wote ni muhimu kwetu…

“Nakumbuka kocha Hall alituambia kuwa kama tunataka kuwa mabingwa ni lazima tuhakikishe tunafikisha pointi 60, tena alituambia akiwa amechora kabisa ubaoni, tukayafanyia kazi na sasa tunaona matunda yake…

Omog naye ana kazi yake nadhani hatujamchukua bure, tunajua ana mafanikio makubwa kwenye michuano ya kimataifa, tuna imani atatuvusha,” alisema.


CHANZO: HABARI LEO

0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.