Monday, August 11, 2014

AZAM FC WAICHAPA KMKM GOLI 4

Posted By: Unknown - 10:25 AM

Share

& Comment

AZAM FC jana ilipata ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya KMKM katika Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame mjini Kigali.

Kwa ushindi huo wa mechi hiyo ya Kundi A, Azam FC imejikusanyia pointi nne na kujiweka pazuri katika kusaka tiketi ya kucheza robo fainali.

Mabingwa hao wa Tanzania Bara msimu wa 2013/14, walianza michuano hiyo kwa sare ya 0-0 dhidi ya Rayon Sport ya Rwanda, Ijumaa iliyopita. Kwa KMKM ambao ni mabingwa wa Zanzibar kwa misimu miwili sasa, imepoteza mechi yake ya kwanza baada ya kuanza na sare ya 1-1 dhidi ya Atlabara ya Sudan Kusini.

Azam FC ambayo inashiriki michuano ya mwaka huu baada ya Yanga kufukuzwa na waandaaji, Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), ilikwenda mapumziko ikiwa mbele 3-0. John Bocco ambaye hakuwa na mechi nzuri dhidi ya Rayon Sport, jana alifunga bao la mapema zaidi katika michuano hiyo hadi sasa baada ya kuunganisha wavuni kwa kichwa mpira wa adhabu ndogo wa Shomari Kapombe katika dakika ya kwanza.

Kama hiyo haitoshi, mshambuliaji kutoka Haiti, Lionel Saint-Preux alifunga bao la pili katika dakika ya 19, akimalizia mpira uliotemwa na kipa wa KMKM, Mudathir Khamis kutokana na shuti la mpira wa adhabu ndogo lililopigwa na Kipre Tchetche.

Azam FC ilipata bao la tatu dakika 10 baadaye, wakati Saint-Preux alipomalizia wavuni kazi nzuri iliyofanywa na Kapombe na Kipre Tchetche.

KMKM inayofundishwa na kocha mzoefu Ali Bushiri, ilikwenda mapumziko ikiwa nyuma kwa mabao hayo, na ilionekana kushindwa kabisa kasi ya Azam FC.

Bocco alihitimisha karamu hiyo ya mabao dakika saba baada ya kuanza kwa kipindi cha pili, safari hii akitumia krosi safi ya kutoka kulia kwa Kapombe ambaye alimegewa pande zuri na Himid Mao.

Azam FC ilianza na kikosi kilichokuwa na badiliko moja kutoka kile kilichocheza na Rayon Sport kwa kumuanzisha Saint-Preux badala ya Mcha Khamis ambaye aliingia kipindi cha pili kumbadili Bocco.
Aidha, David Mwantika alimpisha Said Moradi na kisha Kipre akatoka na kuingizwa Didier Kavumbagu.

Kiungo nyota wa Azam FC, Salum Abubakar alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo na kutamba kuwa timu hiyo itashinda mechi zote na kutawazwa mabingwa wapya wa Kagame. Kwa upande wake,

Bushiri alisema bao la mapema liliwachanganya wachezaji wake na pia kikosi chake bado kina damu changa, hivyo kinajifunza.

Katika mechi ya kwanza jana, KCCA ya Uganda baada ya kuilaza Gor Mahia kwa mabao 2-1, ilikutana na kipigo kama hicho kutoka wa Telecom ya Djibouti. Jioni jana, Rayon iliikabili Adama ya Ethiopia.

Michuano hiyo inaendelea leo kwa mechi nyingine tatu kati ya Banadir dhidi ya El Merreikh, Gor Mahia dhidi ya Atletico na Vital’O itaikabili Polisi ya Rwanda.
Mshambuliaji wa Azam FC, Didier Kavumbangu akimtoka beki wa KMKM katika mchezo wa Kundi A, Kombe la Kagame jioni ya leo Uwanja wa Amahoro, Kigali, Rwanda. Azam ilishinda 4-0.
Beki wa KMKM akimvuta beki wa Azam, Shomary Kapombe kumpunguza kasi
Mshambuliaji wa Azam FC, John Bocco akiwafunga btela mabeki wa KMKM
Beki wa KMKM, akimpunguza kasi mshambuliaji wa Azam FC, Kipre Tchetche
Kipre Tchetche alikuwa mwiba kwa mabeki wa KMKM leo
Beki wa Azam FC, Aggrey Morris akigombea mpira wa juu dhidi ya wachezaji wa KMKM
Mshambuliaji wa Azam FC, Leomel Saint-Preux akiwachambua mabeki wa KMKM
Leonel Saint-Preux akimtoka beki wa KMKM


0 Maoni:

Post a Comment

Copyright © CHAMA LANGU NI AZAM FC™ is a registered trademark.

Designed by Templateism. Hosted on Blogger Platform.